Ujumbe na matashi mema kwa Askofu mkuu mteule Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Jumuiya
ya Waanglikani Duniani
Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja miongoni mwa
Wakristo, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemtumia ujumbe
wa matashi mema, kheri na baraka, Askofu mkuu mteule Justin Welby wa Jimbo la Durham
ambaye hivi karibuni ameteuliwa na kuthibitishwa na Malkia wa Uingereza kuwa Askofu
mkuu mteule wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza na Kiongozi mkuu wa Jumuiya wa Anglikani
Duniani.
Kardinali Koch anasema, uhusiano kati ya Kanisa Anglikani na Kanisa
Katoliki ni muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, changamoto kwa
wakristo kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo anayewataka wafuasi wake kuwa wamoja
kama ambavyo anabainisha katika ile sala ya kikuhani.
Kwa takribani miaka
hamsini iliyopita, Makanisa haya mawili yameendelea kujikita katika majadiliano ya
kiekumene katika ngazi ya kitaalimungu, kwa kutafuta muafaka unaopania kuwasaidia
waamini wa Makanisa haya kufahamiana kwa karibu zaidi.
Katika kipindi hiki
chote, Mapapa na Wakuu wa Kanisa Anglikani wamekutana na kuzungumza mara kwa mara,
kwa pamoja wamekazia urafiki wao katika maisha ya kiroho na kiutu pamoja n akutambua
changamoto iliyoko mbele yao ya kutaka kutolea kwa pamoja ushuhuda wa imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake na huduma kwa Jamii inayowazunguka.
Ni matumaini ya Kardinali
Koch kwamba, urafiki huu utaendelezwa na kwamba, kwa wakati muafaka atajitahidi kutafuta
nafasi ya kuweza kukutana naye ana kwa ana kwa ajili ya majadiliano ya pamoja yanayopania
kudumisha umoja wa kikristo, ili ulimwengu uweze kuamini. Anapenda pia kumhakikishia
sala zake anapotekeleza wajibu na dhamana aliyokabidhiwa kwa Kanisa Anglikani.