Hotuba ya Rais Kikwete wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 8 wa CCM, Dodoma
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa
kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku ya leo tarehe 11 Novemba
2012, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru
Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu,
niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa
na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema
Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na
kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo Makao
Makuu ya nchi yetu na Chama chetu. Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi
hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano
huu wa Nane wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri
Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati
zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano
huu kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana. Ndugu Wajumbe;
Karibuni
tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi
wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu
kuliko nilivyotazamia. Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio
yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Lakini tukaona
ni mbali mno na walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club
ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo
la Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati
ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo
asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention
Centre). Baadae utafuata ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli
ya Kisasa.
Wageni Karibuni Ndugu Wajumbe; Kama mjuavyo
Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko duniani. Tumekuwa na
mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu. Safari hii tumefanya hivyo tena.
Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki
Afrika na duniani kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo
kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu
ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru
Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki
nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu. Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha
kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini
kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya
leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha
jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru
sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi. Kuwepo
kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na kuupa
baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea
mema Chama chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora Ndugu
Wajumbe; Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu
waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao
kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa wanastahili pongezi
maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape
makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano Ndugu Wajumbe; Agenda ya Mkutano
Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina mambo makuu manne. Kwanza kufanya
marekebisho ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana
na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili
2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa
kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho
ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi
kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu
Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za
maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi
mkuu hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi
za Chama kwa miaka mitano iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi
wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania
Bara.
Ndugu Wajumbe; Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa
inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili
taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani. Kisha kila kikundi kitatoa
taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa
kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu
mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa
zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu Ndugu Wajumbe; Katika
hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006,
pamoja na kuzungumzia mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu.
Nilitoa maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika
ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya hivyo kwa sababu
hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na
kila mwanachamawa CCM. Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi
lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai
wa Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama chao.
Ndugu Wajumbe; Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu
wa CCM, Ndugu Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa
Kuimarisha Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi
za Chama tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na
kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia
utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa
tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya uimarishaji
wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.
Ndugu Wajumbe; Kazi ya kuimarisha
Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM, kila kiongozi wa CCM na
kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo, Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa
na ukomo. Ni kazi ya kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt.
Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi
ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa Chama cha Mapinduzi. Hii
siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo
kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati
wote tuwe tunaingiza wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa
na Katiba ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli
na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu
Wajumbe; Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima Chama chetu
kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na kukipigania.
Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama chetu ina maana ya kuwa
na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa dola. Pia wanachama ni nyenzo
muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya
ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma. Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi
ya kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi
za uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri Ndugu Wajumbe; Kazi ya kuhakikisha
kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa
kuchuja majina ya wagombea. Lazima Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini
wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali
zake. Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi.
Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo
Chama chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni maamuma.
Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha
Mapinduzi na kama hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na kiongozi ambaye
haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi ya Chama ni
sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe
anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba.
Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme, tuwashughulikie,
wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu Wajumbe; Kiongozi mzuri wa CCM
lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na jamii imuone hivyo. Chama
chetu kinashindania kushinda akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia
kiongozi wetu afanye katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma. Lakini,
ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu
muhimu. Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama jamii inamuona kuwa si mtu
muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo
ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke
kuwa balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu Wajumbe; Baada ya kukamilisha mchakato
wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo
kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza
na kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha
kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa
inafanywa katika Chuo cha CCM cha Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu
Wajumbe; Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini
mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada
wa vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu
mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa. Tuko
tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.
Vikao
Vifanyike Ipasavyo Ndugu Wajumbe; Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama
na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa
vizuri na ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni muhimu
kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba mafunzo tutakayotoa
kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia
sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri Ndugu Wajumbe; Kwa Chama
chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala. Lazima tuwe na watendaji
ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa
mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia,
wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya.
Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa kazi hizo. Ni muhimu sana
tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya
Chama chetu kuwa imara. Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi
wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka
mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi kuwa tutaboresha maslahi
ya watumishi wa Chama. Tumetimiza ahadi hiyo. Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea
kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee Ndugu
Wajumbe; Lazima Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha.
Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi. Hivi sasa hatuko hivyo. Hatuna budi kuongeza
maarifa na juhudi za kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali
kama kuna ruzuku au hakuna. Jambo hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha
linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi zote. Kila mmoja afikirie nini cha
kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia ni kufanya shughuli halali. Fursa zipo
tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM.
Lazima tushinde. Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi kuimarisha
usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata
gari mpya tena gari nzuri na imara. Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika
uchaguzi ujao bila ya taabu. Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari
iko mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu.
Jumuiya
za Chama Ni wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake zinaimarika
na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya ndiyo mkono mrefu wa Chama cha Mapinduzi
kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale ambao si wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha
kuwa watu hao wanakuwa wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo
kwa Jumuiya ni fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili
wakati wa uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya lazima zihakikishe
kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii adhimu.
Ndugu
Wajumbe; Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa kuimarisha
Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu wa kila mmoja kufanya.
Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha
kuwa kila mwanachama na kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi
Ndani ya Chama Ndugu Wajumbe; Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi,
Chama cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri
Kuu ya Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama. Lengo
kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira inayovutia katika mitazamo
na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe
Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania.
Tunataka wanawake na wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na
wenye nguvu waone kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe; Kwa ajili
hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:- 1. Kukiwezesha
Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa
Chama chao; 2. Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na
kusukuma mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu; 3. Kukiwezesha Chama kuwa
na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama
na wananchi; 4. Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze
kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima; 5. Kukiwezesha Chama
kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na kuwezeshwa
kutekeleza majukumu yao; 6. Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi
na kupambana na propaganda chafu za vyama vya siasa; na 7. Kukiwezesha Chama
cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la
rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe; Katika mkutano wa Halmashauri Kuu
ya Taifa iliamuliwa kuwa kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani
ya Chama utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka mtakumbuka kuwa
katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya. Vile vile
iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika muundo wa Chama na moja ya matokeo yake
ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani. Nafasi za NEC
za mikoa zikafutwa na zile za taifa zikapunguzwa. Aidha, limeundwa Baraza la Taifa
la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama wastaafu. Wanapata fursa
ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu Wajumbe; Tuliamua,
pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya zifanyike mwaka mmoja. Shabaha ya uamuzi
huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa
kwa chaguzi za dola. Uamuzi huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia
kwa uchaguzi. Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana
na mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe. Lengo ni kuziwezesha
ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe; Suala
la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa sana kwa sababu ya umuhimu
wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya jamii na wanachama wake. Pia, kutokana na
ukweli kwamba ni kilio cha wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya
dhidi ya Chama iliyopo katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni
kilio cha dhati kwa watu wenye nia njema na CCM: Chama chao, wanachokipenda na kukiamini.
Chama ambacho bado hakina badala yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake.
Halmashauri
Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike. La kwanza, mfumo mzima wa kushughulikia
masuala ya usalama na maadili katika Chama utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama
kichukue hatua na lazima kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama
wasiokuwa waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya jamii.
NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo vikao husika katika Chama
vichukue hatua.
Ndugu Wajumbe; Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa
yafanyike katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo
yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa. Yapo mambo mengi ambayo ni endelevu
kama vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi kuendelea kulikemea na kusimama
kidete kupambana na tatizo hili mpaka likomeshwe. Ni kwa maslahi na heshima ya Chama
chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari
kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi Ndugu Wajumbe; Mara
ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi na Dkt. Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera
ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia
tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari
Kuu ya Taifa ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa
nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote
hizo za juu za uongozi wa taifa letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo,
tumeunda Serikali zote mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea
vizuri.
Ndugu Wajumbe; Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa
Kitaifa na mambo yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa
Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif
Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd. Tunawapongeza sana kwa mafanikio
yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee
kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu Wajumbe; Uchaguzi
uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea
wala kujiandaa nazo. Zinaelezea matokeo tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa
makini zaidi katika uchaguzi ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja
lililo dhahiri ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha
kukabili changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo, mbinu hasi
zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa
na mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa
katika Mkutano huu. Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni
Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda kuongeza kwa kusema kuwa
Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe; Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada
ya mkutano tukumbuke na kuzingatia Umoja. Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke.
Tuimbe Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu kuwa: Umoja
ni Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda kuona
kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana na tulioshikamana.
Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba upande mmoja badala
ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli, matendo au watu wanaopandikiza
chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama chetu na miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu
ya ujumbe wa Mkutano huu uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa
watu tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala kuwatafutia
ushindi wagombea wa Chama chetu. Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao:
“vita vya panzi furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama
chetu kiwe hivyo.
Ndugu Wajumbe; Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta
uongozi ndani ya Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo
chanzo kikuu kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu. Hili
ndugu zangu siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya msingi ya mwanachama
na raia wa Tanzania. Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki
yake hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi, vitendo viovu au njama za kuhujumiwa? Nani
mwenye haki zaidi ya mwanachama ama raia mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa
na msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka. Watu wa namna hiyo
ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama chetu kizuri kama tamaa
zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe; Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale
wote wanaochukiana kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo
siyo sahihi, wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa za ngazi
zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba wahusika watoe ushirikiano
wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki katika uchaguzi, walidhulimiwa au
hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu
wa kushughulikia malalamiko yao. Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya vitendo
vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika vyombo vya habari, kufanya
ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe; Niruhusuni
nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya kugombea uteuzi ndani ya Chama
wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa
ni haki ya mwanachama na ni haki ya raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na
gumu kulivumilia ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu. Kuwalazimisha
au kuwashinikiza kujiunga na kundi fulani siyo sawa. Kumchukia mtu kwa sababu naye
anagombea au amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya
demokrasia iwe haina maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni kutumia
fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au kumuunga mkono mgombea
wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni utovu wa maadili usiokubalika
ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita kwa nguvu zetu zote. Naomba wote
tushirikiane katika mapambano haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi Ndugu Wajumbe; Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa
na Waziri Mku, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu. Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo
nizungumzie baadhi ya mambo yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama Ndugu
Wajumbe; Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama pamoja na kuwepo
matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna tishio lo lote la kiusalama
la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi uko salama pamoja na kuwepo kwa
maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili kutofautiana wapi ulipo mpaka halali. Hakuna
jambo lo lote linalofanywa upande wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya
usalama wa nchi yetu kuwa hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza Majeshi
yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na kushushuliwa.
Ndugu
Wajumbe; Tumeendelea na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
kwa kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita. Lengo letu ni kukuza nguvu
ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake kivita. Hali kadhalika, tumeendelea
kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa
upande wa usalama wa raia, yaani maisha na mali zao, matukio ya uhalifu yanaendelea
kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri. Kama tufanyavyo
kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa
vya kisasa vya kufanyia kazi. Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia
kazi na ya kuishi ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe; Pamoja
na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la kigaidi, wakati wote vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya tahadhari kuepuka kushtukizwa. Kama
mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu
11 walipoteza maisha. Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya.
Aidha, tuko katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari
Kuu ya Hindi. Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa nyara meli
katika bahari yetu . Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini yanasikitisha na
kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu ya kuheshimiana na kuvumiliana
pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini, kabila rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo
havikubaliki na Serikali haitawavumilia au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na
kuchochea vurugu hizo. Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi.
Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini
zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana.
Tusipofanya hivyo nchi yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo.
Ndugu
Wajumbe; Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi. Kwa
sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi yetu hawajafanikiwa
kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo
huo huo na sisi katika Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka
kutuvurugia amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe; Napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha
sifa yetu ya kuendeleza utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala
wa sheria. Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa mihimili
mikuu ya dola. Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri.
Muungano
Imara Ndugu Wajumbe; Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye
lengo la kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini hasa
kule Zanzibar. Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na ghasia
ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono. Njia hizo hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha
mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba. Kama mtu ana maoni yo
yote kuhusu Muungano ayafikishe tu, yatapokelewa na kupimwa. Vile vile Kamati ya
Pamoja ya Serikali zote mbili inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya
kazi nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu analo jambo analotaka lipatiwe jawabu
awasilishe kwa wahusika litashughulikiwa.
Hali ya Uchumi Ndugu
Wajumbe; Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio
tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa nchi yetu na
kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea kupambana na changamoto zilizokuwa
mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo
na sisi pia tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika
safari yetu ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu
hiyo, tunatarajia ifikapo mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini
sana duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani tunataka pato la wastani la Watanzania
litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani 3,000.
Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa Serikali na
sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya viongozi na wananchi
wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe; Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza.
Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa
pili ni Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu
na ushindani kimataifa. Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa kipaumbele
katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma. Katika
kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa kwani lengo letu ni kuwa
na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya watu. Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo
wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka wa
jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu. Mauzo yetu ya nje yanazidi kukua na
kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa
ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola
za Kimarekani bilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu
Wajumbe; Changamoto kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua
kutoka asilimia 19.8 Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua
huko ni kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko
wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana EWURA
kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
Kwa kuwa bei za
vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa mfumuko wa bei na kuongeza
gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa
kuagiza bidhaa hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi.
Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo ili nchi
yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje. Hayo ndiyo malengo
na hatua zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea
kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini.
Mapato
na Matumizi ya Serikali Ndugu Wajumbe, Tunazidi kupata mafanikio ya kutia
moyo kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi
Mwezi Agosti 2012, kwa mfano, yalifikia shilingi bilioni 554.8 ikilinganishwa na makusanyo
ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi za
dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo na taasisi
za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko
kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka
2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango
wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka
2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua kutoka
asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21.
Ndugu Wajumbe; Sambamba na kuongeza
mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za umma vinazidi kuimarika.
Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na
Serikali za Mitaa. Pia ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma.
Hati Chafu katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi
kila mwaka. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika
na kazi iliyofanyika au huduma iliyotolewa.
Uwekezaji Ndugu Wajumbe, Serikali
imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara hapa
nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuongeza vitega uchumi nchini
na kupanua biashara ndani ya nchi na kati ya nchi yetu na nchi nyingine duniani.
Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo
uwekezaji unaongezeka. Takwimu zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka
hadi mwaka katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha, ujenzi na sasa
kwenye utafutaji wa gesi na mafuta.
Tumepata mafanikio makubwa katika
utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi. Mwaka 2011,
kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni
7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000. Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza
kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu
kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji
kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Ili kufanikisha hayo, tutaendelea kuboresha
miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na teknohama.
Miundombinu Ndugu
wajumbe; Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza ni kuboresha
miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini. Tumethibitisha hayo kwa
mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo miundombinu ni ya pili baada ya elimu.
Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha
na elimu yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24, na afya yenye shilingi
trilioni 1.5 sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua
mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri
unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua, shughuli za uzalishaji
viwandani na kilimo zinaimarika. Ni kichocheo kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali
za uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini
na vijijini.
Ndugu Wajumbe; Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa
barabara kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa
barabara zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu
mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami
na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake
unakwenda vizuri. Tumeanza kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa
haifikiki kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe
25 Juni, 2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora
kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara katika Mikoa hiyo
tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo na kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe
ni mashahidi. Karibu tunafikia ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe; Inafurahisha zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama
za ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe. Aidha, uwezo wa
Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka sana kutoka shilingi bilioni 58 mwaka
2005 hadi shillingi bilioni 430. Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati
barabara mbalimbali nchini. Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye Halmashauri
zote nchini. Ndugu Wajumbe;
Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha
viwanja vya ndege, bandari na usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza
katika utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za ujenzi
na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na uwezo wetu. Tunaendelea
kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu Ndugu wajumbe; Tumefanikiwa kupanua sana fursa za kuwapatia
elimu vijana wetu katika ngazi zote. Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa
elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha.
Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2015 kama
ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari,
wananchi na wadau wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya
sekondari. Kwa sababu hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa
na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005
hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu.
Hivi sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya
166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa mwaka 2005. Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi
wote tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iwape wanafunzi
wengi mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 56.1
mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu. Wanafunzi wanaopata mikopo wapo
93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie
wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe; Upanuzi mkubwa wa elimu
katika ngazi zote nchini umezua changamoto mbalimbali kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua
changamoto hizo kuwa ni pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi;
upungufu wa vifaa vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini.
Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo. Tumeongeza
vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu. Bajeti ya elimu
ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa
vya kufundishia na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi karibuni nilipokuwa
Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuhakikisha kuwa shule
zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya sayansi katika miaka miwili
ijayo.
Afya Ndugu wajumbe; Suala la afya ya Watanzania tunalipa
umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005
hadi shilingi trilioni 1.5 mwaka huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza
Sera mpya ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM)
wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia Watanzania
huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa tano. Vile vile, ni kuimarisha
huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili.
Katika mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu
wa madaktari, wauguzi na wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu
hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na tutaendelea kujenga
vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua vilivyopo. Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana
na maradhi makubwa yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi yanayoambukiza
kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale yasiyoambukiza kama vile saratani,
moyo, shinikizo la damu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa
miaka mitano. Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea
kupatikana. Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia
5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa
Zanzibar tunakaribia kutangaza kufutika kwa maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu
maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza
na kutibu maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi tunayopeleka
wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari ni hatua, naamini tutafika
kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji Ndugu wajumbe; Tunaendelea
kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini. Tumeanza safari ya uhakika
ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji. Tunapanua umeme utokanao na vyanzo
vingine hasa gesi asilia na makaa ya mawe. Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya
jua nayo iko mbioni. Pamoja na hayo tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa
kwa kutumia mafuta kwa kubadili mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi
majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Litakapokamilika
nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina
wa mgao na upungufu wa umeme nchini. Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa umeme
nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka
asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo
2015.
Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama
zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza ni ule ukweli kwamba
kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo vya maji karibu au hayapati mvua
za kutosha au yana ukame. Katika maeneo ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida
sana na hivyo kutulazimisha kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu.
Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa miradi mingi inayohitaji
pesa nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kufuatia
utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini
na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama. Ni matumaini yangu
kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia
90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa
katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika tutafikia lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi
kwa Kuchaguliwa Ndugu Wajumbe; Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume,
Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa
upande wa Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu Dkt.
Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Ndugu
Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua nafasi hii kwashukuru kwa dhati
Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia
kuongoza Chama chetu. Wamekifanyia Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi
kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa mambo
mengi ya Chama na nchi. Nawashukuru sana. Sote tuwatakie afya njema na maisha marefu.
Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke kuandika vitabu ili hazina yake kubwa ya uzoefu na
maarifa iwanufaishe wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya
na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni
kwa magumu ya uchaguzi mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya
kujenga Chama. Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba nyufa
za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi. Kumbukeni wosia wa
Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni
Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa maslahi
ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho Ndugu Wana-CCM; Kwa kuhitimisha
naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ujenzi wa Chama
na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Bado kazi kubwa
iko mbele yetu kwa mambo yote hayo mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti
ya kutekeleza majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia
malengo yetu. Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM
umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika! Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi Asanteni sana kwa Kunisikiliza