Elimu inayotolewa na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu inapaswa kujikita katika
kufundisha, kutafiti na huduma kwa jamii
Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge, MWUCE, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania, hivi karibuni, kilisherehekea mahafali yake ya tano
kwa kutoa Shahada ya kwanza ya ualimu kwa wanafunzi 591 na wengine 12 walipokea cheti
katika masomo ya sayansi ya Computer kutoka Chuoni hapo.
Katika mahafali yao,
Askofu John Ndimbo, mwenyekiti wa Idara ya Elimu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
alisema kuna haja kwa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu nchini Tanzania kujikita
zaidi katika maboresho katika ufundishaji, tafiti na huduma za kijamii, ili wahitimu
hao wanapotoka vyuoni waweze kuwa wamepikwa barabara kwa ajili ya maendeleo ya Jamii
inayowazunguka.
Ni jukumu la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge kuwaelimisha
wanachuo wake, ili watambue malengo ya elimu inayotolewa hapo Chuoni. Kanisa na Jamii
inawekeza ili kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanapohitimu waweze kutoa huduma bora
zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote.
Askofu Ndimbo amewataka
wahitimu hao kuhakikisha kwamba, wanajikita katika tafiti za kisayansi, ili kuweza
kumwendeleza mtu mzima na kwamba, mwelekeo huu utaiwezesha Tanzania kuendelea kucharuka
katika sekta ya elimu. Amewakumbusha kwamba, tafiti za kisayansi zina madai yake,
zinahitaji nidhamu, uwajibikaji na majitoleo; inawahitaji watu wenye uwepo mpana na
wenye mang’amuzi katika kupembua na kuainisha mambo, ili kweli tafiti hizi zinazofanywa
na wasomi hao ziweze kuleta manufaa kwa Jamii ya watanzania na katika mfumo mzima
wa elimu.
Kwa upande wake, Askofu Isaac Amani, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu
Kishiriki cha Mwenge, Moshi katika hotuba yake, amewataka wahitimu kukuza na kuendeleza
kipaji cha ugunduzi wanapotekeleza majukumu yao kama wasomi na kundi muhimu sana katika
maendeleo na ustawi wa Jamii. Anasema, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mwenge kitaendelea
kutoa elimu kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa na Mama Kanisa pamoja na
Chuo Mama cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT.
Askofu Amani ameiomba
Serikali ya Tanzania, kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Chuo Kikuu Kishiriki
Mwenge katika mchakato unaopania kuhakikisha kuwa kuna idadi kubwa zaidi ya wanafunzi
wanaojiunga na kuendelea na masomo yao ili kuleta maboresjho makubwa zaidi katika
sekta ya elimu, changamoto inayoikabili Tanzania kwa sasa.
Ameiomba Serikali
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi
kwa ajili ya maendeleo ya nchi, kuliko mwelekeo uliopo sasa ambao unawafanya wanafunzi
wengi kuogopa masomo ya sayansi, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa jamii kwa sasa na
kwa siku za usoni.
Askofu Amani anasema, elimu itakuwa na mafunaa pale tu,
itakapozingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa. Ni jukumu kwa wahitimu
kutambua dhamana na wajibu pamoja na kukidhi mategemeo ya jamii inayoendelea kuwekeza
kwa vijana wake kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Jamii ya watanzania katika ujumla
wake, ina imani na matumaini makubwa kwamba, baada ya masomo yao wataweza kutekeleza
majukumu yaliyoko mbele yao kwa nidhamu na majitoleo makubwa.
Kwa upande wake,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki Mwenge Dr. Philbert Vumilia, amesema, mfumo wa
kuwapima wanafunzi unaotolewa na Chuo hiki unawawezesha wanafunzi kujijengea uwezo
na hali ya kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao kama wataalam katika sekta
ya elimu.
Amewataka wahitimu kuwa na upeo mpana zaidi katika ulimwengu huu
wa maendeleo ya sayansi na teknolojia na kutumia kwa busara zaidi kila fursa inayojitokeza
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Jamii kwa
ujumla wake.
Chuo Kikuu Kishiriki Mwenge ni mahali ambapo wanafunzi wanafurahi
kusoma kutokana na juhudi, bidii, maarifa na majitoleo yanayojionesha miongoni mwa
wakufunzi na wanafunzi katika ujumla wao. Kwa mwanafunzi anayetaka kusoma, Chuo Kikuu
KishirikiMwenge ni mahali pake kabisa. Chuo kitaendelea kuwekeza katika maboresho
ya miundo na programme za masomo ili kuinua kiwango cha elimu nchini Tanzania.
Kwa
namna ya pekee, upendeleo unatolewa kwa wanawake na wasichana wanaotaka kujikita katika
maboresho ya maisha na familia zao, ili kupata watu ambao watakuwa wameiva kitaaluma,
kimaadili na kiutu, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo endelevu
ya Jamii ya watanzania. Kwa pamoja, Mwenge inapania kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa
ni mwanga na nuru ya ulimwengu.
Mgeni rasmi katika mahafali haya alikuwa ni
Mheshimiwa Philip Mulugo, Naibu Waziri wa elimu na mafunzo, ambaye amepongeza juhudi
na mchango unaotolewa na Chuo Kikuu Kishiriki Mwenge katika sekta ya elimu