Baraza la Makanisa Ulimwenguni lampongeza Askofu mkuu mteule Justin Welby
Dr. Olav Fyskse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, amemwandikia
salam na matashi mema, Askofu mkuu mteule Justin Welby wa Jimbo la Durham, Kanisa
Anglikana kwa kuteuliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Jumuiya Waanglikani Duniani. Anakumbusha
kwamba, Kanisa Anglikani ni kati ya wanachama waasisi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Askofu mkuu mteule anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Rowan Williams
wa Cantebury ambaye anang’atuka madarakani na anatarajiwa kufundisha Chuo Kikuu cha
Cambridge, kilichoko Uingereza.
Katibu mkuu kwa niaba ya Baraza la Makanisa
Ulimwenguni anapenda kuchukua fursa hii kumkaribisha kwa kutambua mchango wa Kanisa
Anglikani katika jitihada za majadiliano ya kiekumene na kwamba, wanatarajia kujenga
na kuimarisha zaidi umoja miongoni mwa Makanisa haya. Dr. Tveit anasema, anatambua
mchango mkubwa ambao Kanisa Anglikani linaendelea kutoa kwa ajili ya maisha na ustawi
wa Kanisa na wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.
Mwelekeo huu unaoneshwa
pia na Askofu mkuu mteule Justin Welby, hasa kwa kutaka kuwasaidia wananchi wa Nigeria
kuvuka vikwazo vya mashambulizi ya kigaidi pamoja na kujenga mshikamano wa dhati kati
ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini humo, kwa njia ya majadiliano ya
kidini yanayopania mafao ya wengi.
Hili ni jukumu ambalo Baraza la Makanisa
Ulimwenguni linapania kuliendeleza katika siku za hivi karibuni nchini Nigeria. Ni
matumaini ya Baraza hili kwamba, Askofu mkuu mteule, ataunga mkono jitihada hizi kwa
ajili ya mafao ya wengi nchini Nigeria na kwamba, atakuwa ni kiongozi wa Kanisa kwa
sasa na kwa siku zijazo.
Dr. Olav Tveit anamshukuru kwa namna ya pekee, Askofu
mkuu Rowan Williams kutokana na mchango wake mkubwa katika maisha na utume wa Baraza
la Makanisa Ulimwenguni uliosimikwa katika urafiki wa dhati. Ni matumaini yake kuwa
wataendeleza urafiki huu hata kwa siku za usoni.