Baa la njaa linawanyemelea watu zaidi ya millioni mbili nchini Angola
Serikali ya Angola hivi karibuni ilitangaza hali ya hatari kutokana na kuongezeka
kwa baa la njaa nchini humo linalowasibu zaidi ya watu millioni mbili na kati yao
kuna watoto laki tano wanaoendelea kusumbuliwa na utapiamlo wa kutisha. Hii ni kutokana
na kukithiri kwa ukame na kwamba, kati ya majimbo kumi na nane nchini humo, majimbo
kumi yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula unaotishia maisha ya watoto zaidi ya
laki tano.
Serikali ya Angola kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ndani
na nje ya nchi wamezindua kampeni maalum inayopania kupambana na utapiamlo wa kutisha
miongoni mwa watoto. Mpango huu, unatarajiwa kuwahudumia watoto wanaoishi kwenye Majimbo
ya Zaire, Bie, Huambo, Kwanza-sul, Cunene, Huila, Bengo, Bengula, Moxico na Namibe.
Mpango huu pamoja na mambo mengina utajenga vituo vya afya pamoja na kuwapatia mafunzo
wahudumu wa sekta ya afya wapatao elfu mbili, ili kusaidia jitihada za kupambana na
utapiamlo nchini Angola.
Ukame wa kutisha kutokana na mvua kutonyeesha kwa
muda mrefu, imepelekea kushuka kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo, ikilinganishwa
na msimu uliopita, kiasi kwamba, usalama wa uhakika wa chakula uko mashakani kwa zaidi
ya watu millioni moja na laki nane. Licha ya utajiri mkubwa wa mafuta unaopatikana
nchini Angola yenye idadi ya watu millioni ishirini, lakini bado baa la njaa, umaskini
na ujinga vinawaandama wananchi wa Angola kwa kiasi kikubwa.