Askofu Beatus Kinyaiya asema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika Uinjilishaji
Mpya na wa kina Barani Afrika
Mababa wa Kanisa wanabainisha kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii ni ulimwengu
unaopaswa kuinjilishwa, ili viweze kuleta msukumo mkubwa zaidi katika jitihada za
Bara la Afrika kujitafutia maendeleo endelevu. Vyombo vya habari vina mchango mkubwa
katika kukuza na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Familia ya binadamu daima
wakipania kutafuta mafao ya wengi.
Teknolojia
ya habari na mawasiliano ilenge pia kukuza na kudumisha haki, amani, umoja na mshikamano
wa kweli. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji
Dhamana ya Afrika anabainisha kwamba, kuna haja ya vyombo vya habari kutumika katika
dhamana ya Uinjilishaji, sanjari na kusaidia juhudi za Kanisa Barani Afrika katika
mchakato unaopania kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho.
Tangu
baada ya maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu Barani Afrika, Majimbo na Mashirika
mbali mbali yameanzisha Radio ili kuimarisha juhudi za Uinjilishaji wa kina. Katika
mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki Mbulu,
Tanzania anasema, Radio Habari Njema inayomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Katoliki
Mbulu, ina mchango mkubwa katika azma ya Uinjilishaji mpya na wa kina, kwa sababu
inaburudisha, inahabarisha, inafundisha, inaonya na kukemea.
Ikumbukwe kwamba,
upashanaji habari ni wito unaopania kuwamegea wengine ile furaha ya Habari Njema inayobubujika
kutoka katika maisha na utume wa Kanisa. Katika utume huu, Kanisa linatekeleza wajibu
huu nyeti likikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha
na rasilimali watu, kiasi kwamba, wakati mwingine haliwezi kukidhi ndoto za wafanyakazi
wake za kupata mishahara minono na marupurupu kibao! Wafanyakazi hawa wanapaswa kutambua
kwamba, Kanisa linathamini sana mchango wao katika Uinjilishaji.
Askofu Beatus
Kinyaiya anawaalika wasikilizaji kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, wanajenga
utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kuacha mtindo wa kubagua vipindi, kwani vyote
vimepangwa kwa ajili ya majiundo ya mzima: kiroho na kimwili. Anawapongeza wamiliki
wa vyombo vya upashanaji habari ambavyo vinaendelea kuongezeka nchini Tanzania kwa
kuthubutu kuwekeza katika sekta hii nyeti, yenye madai ya rasilimali watu, fedha na
muda.
Anasema, changamoto na ugumu wanaokutana nao visiwakatishe tamaa, bali
wasonge mbele wakipania kuboresha huduma yaokwa jamii, kwa kuzingatia mafao ya wengi,
misingi ya haki, amani, utu na maadili mema. Matatizo na changamoto zinapojitokeza
zitafutiwe dawa ili vyombo hivi viendelee kutoa huduma kwa Jamii husika.