Watoto wana haki ya kuwa na Baba na Mama katika Familia!
Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican katika tahariri yake anabainisha
kwamba, kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio makuu matatu yanayojikita
katika suala zima la ndoa. Mahakama kuu nchini Hispania imetupilia mbali rufaa iliyokuwa
inataka sheria kutambua kwamba ndoa inaundwa na uhusiano kati ya mume na mke, badala
ya kuachia mahusiano haya kuwa ni kati ya watu wawili.
Nchini Ufaransa, Serikali
imepeleka muswada unaowataka wabunge kujadili na hatimaye kubadili sheria kuhusu ndoa
ili kuwashirikisha pia watu wa jinsia moja wanaotaka kuishi pamoja kama Bwana na Bibi.
Nchini Marekani, kuna baadhi ya sheria ambazo zimefanyiwa marekebisho wakati wa pilika
pilika za uchaguzi mkuu nchini humo uliohitimishwa hivi karibuni ili kutoa mwanya
kwa watu wa jinsia moja kuungana pamoja kama Bwana na Bibi.
Padre Lombardi
anasema kwamba, hii kimsingi si habari, kwani tangu mwanzo, watu wenye mapenzi mema
walitambua mwelekeo kama huu, lakini jambo la msingi ambalo watu wanapaswa kujiuliza,
Je, mabadiliko yote haya yanamlenga nani? Je, ni kwa ajili ya mafao ya wengi ndani
ya Jamii? Huu si msimamo wa Kanisa Katoliki peke yake, hata Rabi mkuu wa Ufaransa
ameonesha kusikitishwa sana na mwelekeo huu. Hili si swala la ubaguzi wa kijinsia.
Hapa ni kutambua kwamba, mtoto anayezaliwa anayo haki ya kuwamfahamu Baba
na Mama yake, ili kuwa kweli na mwono chanya kuhusu maisha ya mwanadamu, utu na heshima
yake, bila kusahau mahusiano yake ndani ya Jamii. Ndoa ya watu wa jinsia moja, anasema
Padre Lombardi si utamaduni unaopaswa kupigiwa debe! Kuna mifumo mbali mbali ya ndoa
ambayo pia si sahihi kwa mfano ndoa za wake wengi.
Kanisa litaendelea kusimama
kidete kulinda na kutetea ndoa kati ya mwanaume na mwanamke kadiri ya mpango wa Mungu
kwa mwanadamu.