2012-11-10 15:45:34

Waimbaji wanayo dhamana ya kutangaza Imani na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwa njia ya karama na vipaji vyao!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe 10 Novemba 2012 alikutana na kufanya mazungumzo na Wanachama wa Chama cha Kitume cha Mtakatifu Cecilia kinachojikita zaidi katika nyimbo zinazohamasisha ushiriki mkamilifu katika Liturujia, wakati wa Kongamano lao kitaifa, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Ni chama ambacho, kimekuwa mstari wa mbele kufundisha kwa namna ya pekee, Katiba ya Liturujia ya Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanapania kwa namna ya pekee kabisa, kuhakikisha kwamba, waamini wanaifahamu fika imani yao kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya na kwamba, Muziki Mtakatifu una sehemu kubwa katika kuimarisha na kuhamasisha shughuli za Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika hotuba yake kwa wanachama hawa, amegusia mchango wa Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, aliyeshiriki kwa kipindi kirefu maadhimisho ya Liturujia yaliyokuwa yanaongozwa na Mtakatifu Ambrose, kwa kusema kwamba, imani kimsingi inazaliwa kutokana na kusikiliza Neno la Mungu katika mapana yake. Kutokana na ukweli huu, nyimbo ambazo zinachota utajiri wake kutoka katika Zaburi na Maandiko Matakatifu kwa ujumla, zina uwezo mkubwa wa kutangaza imani pamoja na kusaidia juhudi za Uinjilishaji, kama anavyoshuhudia Mtakatifu Agostino.

Itakumbukwa kwamba, anayeimba vizuri huyo anasali mara mbili, ndiyo maana Mtakatifu Ambrose alitoa kipaumbele cha kwanza kwa kukuza na kuimarisha muziki mtakatifu wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Ushuhuda wa Mtakatifu Agostino anasema Baba Mtakatifu uwe ni ushuhuda makini katika harakati za Mama Kanisa kwamba, Muziki mtakatifu, ukiambatana na maneno ni sehemu ya Liturujia ya Kanisa, inayoweza kuboresha imani na hivyo kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani; hatima yake, ni kwa ajili ya kuwatakatifuza Watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa namna ya pekee, anawashukuru na kuwapongeza Wanakwaya wanaotumia vyema vipaji na karama zao kwa ajili ya kuhamasisha Liturujia ya Kanisa, ili waamini wanaposhiriki katika ujumla wao, waweze kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na heshima; wakitambua daima kwamba, kwa kuimba wanasali na kuwafanya wengine kushiriki katika sala hii, ili kwa pamoja Mwenyezi Mungu aweze kupewa sifa anayostahili.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya Nyimbo na Uinjilishaji Mpya; changamoto ya kuthamini na kuenzi nyimbo mbali mbali zinazotungwa hata katika Makanisa machanga duniani. Kwa njia ya nyimbo watu wanaweza kugundua uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao, wanaweza kutubu na kuongoka pamoja na kuimarisha imani yao.

Nyimbo zilizotungwa kwa ufasaha na ustadi mkubwa zina mvuto na mguso katika akili na mioyo ya watu, changamoto kwa watunzi, wanamuziki na waimbaji wenyewe kutambua dhamana na mchango wao katika maboresho ya Liturujia, bila kusahau kuthaminisha utajiri wa nyimbo za Kanisa kama ambavyo Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kuhimiza.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawahimiza waimbaji kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha Watu wa Mungu katika Liturujia kwa kusikiliza na kushiriki kikamilifu, ili kwa njia ya vipaji na karama zao, waiwezeshe mioyo ya waamini kuimba wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.