2012-11-10 08:26:25

Seminari ni mahali ambapo imani inaungamwa, inaadhimishwa, inamwilishwa na kusaliwa! Ni Chemi chemi ya hekima na Utakatifu wa maisha!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Ijumaa, tarehe 9 Novemba, 2012 alikutana na kuzungumza na Majandokasisi wa Jimbo Katoliki la Owerri, Nigeria, kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Kikao cha Hekima, mahali ambapo, Jimbo zima linawatuma wanafunzi wake mahali hapa ili kupata majiundo na malezi ya maisha na wito wa kipadre.

Kardinali Filoni aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Kanisa la Mtakatifu Yohane wa Laterano, lililoko mjini Roma. Amewakumbusha Majandokasisi kwamba, ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayewakirimia neema na baraka ili kuweza kuwa vyombo madhubuti kwa ajili ya utume wa Mama Kanisa pamoja na kuimarisha ushuhuda wao. Anawaalika walezi wa waseminari kuhakikisha kwamba, wanakuwa wazi kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, ili waweze kukidhi matamanio ya binadamu kutoka kwa Mapadre wao.

Kardinali Filoni anakumbusha kwamba, wito na maisha ya Kipadre ni zawadi kutoka kwa Kristo mwenyewe inayopokelewa kwa moyo mkuu na uchaji. Seminari ni mahali ambapo Majandokasisi wanapata majiundo makini wakiongozwa na Roho Mtakatifu, ili kujiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Ili kufanikisha wito huu, kuna haja kwa Waseminari kuhakikisha kwamba, wanajishikamanisha na Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yao, ili waweze kutambua nia ya Roho Mtakatifu katika ujana wao.

Seminari inapaswa kuwa ni mahali pa kujifunza hekima na utakatifu wa maisha na kwamba, kipindi chote cha majiundo ni fursa makini inayopania kuandaa mihilimi ya Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwapatia mbinu mpya, ari na nguvu ya kuweza kutekeleza wajibu wao msingi kwa Familia ya Mungu inayowasubiri kwa hamu kubwa.

Ujumbe huu unasimikwa kwa namna ya pekee katika Yesu Kristo, aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Majiundo ya Majandokasisi yanasimiwa katika nguzo kuu nne nazo ni: maisha ya kiutu, kielimu, kiroho na kichungaji. Kila nguzo ina umuhimu wake katika majiundo ya Waseminari, ili kuweza kufikia ukomavu na kuwa ni madaraja ya watu wanaotamani kukutana na Yesu Kristo.

Kardinali Filoni anawakumbusha Makleri kwamba, watu wanawasikiliza kwa umakini mkubwa kwa sababu wao ni mashahidi amini wa Yesu Kristo, wanayemuungama kwa vinywa vyao, lakini zaidi, kwa njia ya matendo yao adilifu. Kutokana na ukweli huu, Jumuiya ya Seminari inapaswa kuwa ni mahali ambapo: imani inaungamwa, inaadhimishwa kwa umakini mkubwa, watu wanajitahidi kuiishi na kuimwilisha katika sala. Imani inakuwa na kuchanua ikiwa kama inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Kardinali Fernando Filoni anasema kwamba, kila Mkristo anaitwa kuwa ni mfuasi wa Kristo, lakini kwa Makleri, wito wao ni alama ya upendeleo wa pekee kutoka kwa Kristo, ili kushiriki katika kuwagawia Watu wa Mungu, Mafumbo ya Kanisa. Changamoto kwa vijana kujitokeza bila woga, ili kutolea maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kwa njia ya maisha na wito wa Kipadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.