"Padre Quadrio alikumbatia ukweli na upendo ili kupata ukweli wa upendo"
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 10 Novemba 2012,
ameshiriki katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 75 tangu Kitivo cha Taalimungu,
Chuo Kikuu cha Torino, kilipoanzishwa na kumbu kumbukumbu ya miaka 50 tangu alipofariki
dunia Mheshimiwa Padre Quadrio, aliyezaliwa tarehe 28 Novemba 1921. Ni mtu ambaye
maisha yake yalitajirishwa na tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisarkamenti na
matendo ya toba, kama sehemu ya mchakato wa hija ya maisha yake kutaka hata yeye siku
moja aweze kuwa kati ya Watakatifu wa Mungu.
Ni Padre aliyekuwa na Ibada ya
pekee kwa Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, akajitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya majiundo ya wanafunzi wake katika Mafundisho tanzu ya Kanisa. Alikuwa
ni Padre aliyetoa mchango mkubwa katika tafakari za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican,
hususan kuhusu mwaliko wa waamini wote kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Alipokea
mateso na ugonjwa wake kwa imani na matumaini makubwa, daima akiendelea kujikita katika
sala.
Kardinali Bertone anasema kwamba, Padre Quadrio alikuwa ni Jaalimu aliyesimama
kidete kulinda na kutetea Injili ya Maisha kwa njia ya ushuhuda wake uliojengeka katika
maahusiano mazuri na watu, kiasi kwamba, akapewa dhamana ya kufanya utume na shughuli
za kichungaji miongoni mwa vijana. Akakuza uhusiano huu katika misingi ya urafiki,
kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wote.
Alikuwa mtu mwema na
mwenye moyo mzuri kwa wote waliokuwa wanateseka katika umaskini na upweke; akaguswa
na mahangaiko yao; akawasikiliza kwa umakini mkubwa na kuwapokea jinsi walivyo, akijitahidi
kuwasaidia kadiri ya uwezo wake. Alipenda pia kutekeleza Mapenzi ya Mungu katika maisha
yake na daima alionesha imani kubwa, kwa hakika anasema Kardinali Bertone, huyu alikuwa
ni Padre na mfano wa kuigwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo
na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.
Aliliadhimisha Fumbo hili kwa Ibada
na uchaji; akalitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume
wake. Injili ilikuwa ni dira na mwongozo wake, kiasi kwamba, alitambulika kuwa kweli
ni mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na Jalimu mahiri la Maandiko Matakatifu na
kielelezo cha utakatifu wa maisha.
Kardinali Tarcisio Bertone anasema kwamba,
dhamana ya Uinjilishaji Mpya inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa sasa lazima iende
sanjari na maisha ya: Sala, tafakari ya kina pamoja na kujenga umoja na mshikamano
miongoni mwa Familia ya Mungu kwa kutambua kwamba, Kanisa hapa duniani linasafiri
kuelekea Yerusalemu ya mbinguni, changamoto ya kuwa kweli ni watu wa Mungu, kwa kukumbatia
upendo na ukweli ili kupata ukweli wa upendo