Mwaka wa Imani uwawezeshe wanafunzi kuwa mashahidi amini wa Kristo na Kanisa lake
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemwandikia ujumbe wa matashi mema, Askofu
msaidizi Lorenzo Leuzzi, wakati huu wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali mjini Roma,
wanapofanya hija ya kichungaji mjini Assisi, Italia, siku ya Jumamosi, tarehe 10 Novemba,
2012, wakiongozwa na kauli mbiu "Alipokuwa angali mbali" inayotolewa kwenye sehemu
ile ya Injili inayomzungumzia Baba Mwenye huruma na Mwana mpotevu.
Baba Mtakatifu
katika ujumbe huu ambao umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu
mkuu wa vatican anabainisha kwamba, leo ya binadamu ndiyo leo ya Mwenyezi Mungu inayojidhihirisha
kwa namna ya pekee, katika maeneo ya Mji wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, shahidi
amini wa Yesu na Injili yake.
Mwanzoni mwa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani,
Baba Mtakatifu anapenda kuwatakia kila la kheri wanafunzi wanaofanya hija hii ya maisha
ya kiroho kwamba, mfano na maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assis, Msimamizi wa Italia,
utaibua kwa namna ya pekee miongoni wa vijana hamu ya kuwa mashahidi waaminifu kwa
Kristo na Kanisa lake, kwa kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inaendelea kuleta
upya wa maisha. Mwishoni, anawatakia kila la kheri na baraka tele katika Mwaka wa
Masomo uliofunguliwa hivi karibuni.