2012-11-10 09:54:13

Kongamano la 23 la Utume wa Bahari kufanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 19 hadi 23 Novemba 2012


Kardinali Antonio Maria Veglio, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, akishirikiana na viongozi waandamizi kutoka katika Baraza lake, Ijumaa tarehe 9 Novemba 2012 wamefanya mazungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la ishirini na tatu la Mabaharia Kimataifa, litakalofanyika hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 19 hadi 23 Novemba 2012.

Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki mia nne na kumi kutoka katika nchi sabini na moja, wakiongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji katika Ulimwengu wa Mabaharia". Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Mwaka wa Imani ni changamoto na fursa kwa wadau wa shughuli za kichungaji kwa mabaharia kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza miongoni mwao, anasema Kardinali Veglio.

Umefika wakati kwa wahudumu hawa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa shughuli zao za kichungaji miongoni mwa mabaharia, ili kuboresha hali ya maisha ya mabaharia, hasa wale wanaofanya kazi kwa njia ya mikataba kiasi kwamba, inawalazimu kutumia muda wao mrefu wakiwa Baharini, mbali kabisa na familia zao. Tatizo hili limekua na kupanuka baada ya baadhi ya wamiliki wa meli kuacha vyombo na mabaharia wao bandarini bila chakula wala fedha za kuweza kujikimu, hali ambayo inawaweka mabaharia hawa katika hatari ya kunyonywa na kunyanyaswa.

Katika miaka ya hivi karibuni anasema Kardinali Veglio, tatizo la uharamia baharini limeongezeka maradufu kiasi cha kutishia usalama wa maisha na mali wanazobeba mabaharia katika vyombo vyao. Ni tatizo ambalo linawaathiri wahusika na familia zao kisaikolojia kiasi cha kuwaachia madonda makubwa katika vichwa vyao.

Jumuiya ya Kimataifa imeliangalia tatizo na changamoto hizi kwa kuridhia Itifaki ya Kazi ya Mabaharia ya Mwaka 2006, inayobainisha kiwango cha chini kabisa kinachotakiwa kwa ajili ya wafanyakazi katika meli za mizigo na kwamba, Itifaki hii inazingatia kwa namna ya pekee haki msingi za Mabaharia.

Utume wa Bahari unaotekelezwa kwa njia ya viongozi wa maisha ya kiroho na watu wanaojitolea, umekuwa ukiwahusisha pia wavuvi pamoja na familia zao. Hadi sasa hakuna takwimu zenye uhakika zinazoonesha ajali wanazokumbana nazo wavuvi hawa, ingawa mashirika mengi ya kimataifa yanaonesha kwamba, sekta ya uvuvi ni kati ya taaluma zenye hatari kubwa kwa wakati huu. Ni watu wanaokabiliwa na sheria dhidi ya uvuvi haramu, wakati mwingine wanakumbana na biashara haramu ya binadamu au kufanyishwa kazi za suluba.

Kwa upande wake, Padre Gabriele Bentoglio, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, alitumia fursa hii kufafanua ratiba na mambo yatakayozingatiwa wakati wa maadhimisho ya Kongamano la ishirini na tatu ya wahamiaji kimataifa. Siku ya kwanza, wajumbe watajikita katika tafakari kuhusu Uinjilishaji Mpya, umuhimu wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Mabaharia Wakristo, bila kusahau waamini wa dini nyingine pamoja na Mabaharia wanaotua nanga kwenye Bandari za Nchi za Kiislam.

Ushirikishwaji wa Sekta ya Bahari ni mada itakayochambuliwa na Katibu mkuu wa Mfuko wa Wafanyakazi wa Bahari Kimataifa, unaovijumuisha vyama vya Mabaharia mia saba na nane, vyenye jumla ya wanachama zaidi ya millioni tano kutoka katika vitengo mbali mbali vya sekta ya usafirishaji duniani. Mfuko huu unashirikiana kwa karibu zaidi na Utume wa Bahari kwani unapania kuboresha maisha ya Mabaharia, kwa kuwapatia huduma ya kwanza pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili.

Wavuvi ni mada itakayopembuliwa siku ya tatu. Utume wa Bahari unapania kutumia siku hii kwa ajili kuhamasisha watu kuridhia Itifaki ya Kazi katika Sekta ya Uvuvi, inayotoa ajira kwa watu zaidi ya millioni thelathini na sita.

Siku ya Nne, wajumbe watajikita zaidi katika kuliangalia kwa namna ya pekee: Uharamia Baharini, tatizo ambalo limekuwa na athari kubwa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi, hususan nchi ambazo ziko kwenye Pembe ya Afrika, Mwambao wa Bahari Afrika Magharibi, Amerika ya Kusini na katika Visiwa vya Caribbean. Hili ni tatizo ambalo limekuwa vigumu sana kuweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, lakini linaendelea kuongezeka siku hadi siku na watu wengi wanatekwa nyara kwa kipindi cha muda mrefu.

Mwishoni, wajumbe wa Kongamano la ishirini na tatu la Mabaharia Kimataifa watachambua kwa kina na mapana utume wao na jitihada za kuendeleza majadiliano ya kiekumene na kidini kwa ajili ya kuwahudumia mabaharia. Ni siku ambayo Haki Msingi za Mabaharia zitawasilishwa rasmi, kwa kuhusishwa na Sheria zinazowalinda Mabaharia pamoja na huduma wanazopaswa kupewa wao na familia zao, wanapotekwa nyara na maharamia.







All the contents on this site are copyrighted ©.