Vyombo vya mawasiliano ya Jamii vina mchango mkubwa katika azma ya Uinjilishaji Mpya
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafadhili wa Radio Maria Poland, waliokuwa wanafanya
hija ya maisha yao ya kiroho hapa mjini Roma. Mahujaji hao walifika Roma ili kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa utume wa Radio Maria nchini Poland kwa takribani miaka
ishirini, radio ambayo kwa hakika imekuwa ni chombo kikuu cha Uinjilishaji Mpya.
Ilikuwa
ni fursa ya kuweza kujifunza kutoka kwa Watakatifu mbali mbali, lakini kwa namna ya
pekee, Mtakatifu Petro na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, ambaye ameitangaza Injili
ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake.
Kardinali Bertone aliwakaribisha
mahujaji hawa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyewachangamotisha
kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya miaka ishirini ya Radio Maria nchini Poland, inakuwa
ni fursa ya kujiimaarisha kiroho, kwa kufanya hija mjini Vatican na katika Nchi Takatifu.
Mahujaji hawa ni kielelezo cha imani ya mtu binafsi na Kanisa katika ujumla wake;
ni mashahidi wa upendo wa Mungu kwa waja wake na alama ya matumaini kwa maisha ya
uzima wa milele, daima wakijitahidi kuongozwa na huruma ya Mungu katika hija ya maisha
yao kuelekea mbinguni.
Kardinali Bertone anabainisha kwamba, imani kimsingi
ni tukio ambalo linamwezesha mwamini kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, ambaye
kimsingi ni njia, ukweli na uzima. Vyombo vya mawasiliano ya Jamii vina mchango mkubwa
katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya. Ameushukuru uongozi wa radio Maria kwa huduma
yake makini katika kipindi cha miaka ishirini ya uwepo wake nchini Poland na kwamba,
kimesaidia kupandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo mioyoni mwa watu.
Ni
Radio ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kukoleza: Moyo na Maisha ya Sala, Katekesi
makini, Utangazaji wa Injili, bila kusahau utoaji wa habari kuhusu maisha na utume
wa Kanisa pamoja na kurusha matangazo ya maadhimisho ya Ibada mbali mbali zinazoendeshwa
na Baba Mtakatifu. Ameitaka radio Maria kuendeleza utume huu makini ndani ya Kanisa
kwa kumtumainia Roho Mtakatifu.
Kardinali Tarcisio Bertone, amehitimisha mahubiri
yake kwa kuwaweka mahujaji hawa chini ya maombezi ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji
Mpya na ya Mtakatifu Petro, ili Radio Maria poland iweze kuendeleza utume wake kwa
ajili ya mafao ya wengi ndani ya Jamii na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa
la kiulimwengu.