Mshikamano wa Papa na wananchi wa Guatemala waliokumbwa na tetemeko la ardhi
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemtumia ujumbe wa upendo na mshikamano
Askofu Rodolfo Valenzuela Nunes wa Jimbo la Vera Paz, Guatemala kutokana na tetemeko
la ardhi lililotokea tarehe 8 Novemba 2012 na kusababisha watu zaidi ya 50 kupoteza
maisha yao na wengine zaidi ya mia moja na sabini kupata majeraha. Zaidi ya wanajeshi
elfu mbili wanaendelea na jitihada za kuokoa maisha ya watu waliofukiwa na kifusi
baada ya tetemeko hilo.
Baba Mtakatifu anasema, amepokea habari hizi kwa majonzi
na masikitiko makubwa, anapenda kuwahakikishia wananchi wa Guatemala walioguswa kwa
namna ya pekee na maafa haya uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anawakumbuka na
kuwaombea wote waliopoteza maisha yao kutokana na tetemeko waweze kupata pumziko la
milele na majeruhi waweze kupona haraka na hatimaye, kuendelea na shughuli zao za
kila siku.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waathirika wa tetemeko hili
wataweza kuonjeshwa upendo na mshikamano wa kweli. Anawataka waamini pamoja na mashirika
ya misaada ya Kanisa Katoliki kuunganisha nguvu zake ili kuwasaidia waathirika wa
tetemeko hili nchini Guatemala.