Matendo ya huruma na ukarimu ni njia makini ya Uinjilishaji Mpya
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, sauti ya Baba Mtakatifu, ninakuleteeni tafakari
Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa maisha yetu. Tayari tuko ukingoni mwa mwaka
wa Kanisa, ni Dominika ya 32 ya mwaka B wa Kanisa.
Mama Kanisa
ametuwekea Neno likitualika kujitoa na kujiaminisha katika Bwana bila kujibakiza,
tukiwa na matumaini na kwa namna hiyo tutajaliwa yale yote mema yatokayo kwa Mungu.
Ujumbe huu tunaupata kwa mifano hai ya wajane wawili wanaokubali mpango wa Mungu na
kutoa kile chote walichokuwanacho, kinyume na matajiri. Matokeo ya tendo lao jema
wanakirimiwa baraka tele katika maisha yao.
Katika somo la kwanza tunamwona
Nabii Eliya akimkimbia mfalme Ahab ambaye alitaka kumwangamiza. Nabii anapokimbia
anakutana na mama mjane ambaye yuko katika taabu ya njaa! Nabii akitambua taabu ya
mama huyu lakini pia akiwa na tumaini katika Bwana, anamwomba maji na kipande cha
mkate.
Mama huyu alikuwa na unga kidogo kiasi cha kutosheleza siku moja kwa
ajili yake na mwanaye, na baada ya hapo kadiri ya mjane basi wangekufa! Lakini kwa
sababu ya tumaini kuu na akisikiliza sala ya msisitizo ya Nabii Eliya anakubali kutoa
kila kitu. Kwa ufadhili huu alioufanya kwa Nabii wa Mungu, mjane huyu anapata chakula
cha kutosheleza maisha yake mpaka njaa itakapoisha katika nchi ile.
Mpendwa
mwana wa Mungu, ukarimu na tumaini la mjane huyu ndio unaozaa matunda mema. Matunda
haya ni baraka na amani itokayo kwa Mungu. Ni alama ya kwamba Mungu huwajali walio
maskini ambao wanamkimbilia na kumtumaini daima katika maisha yao. Mungu huwajali
wale wote ambao wanakubali kushirikisha vipaji vyao na kugawana mali zao na wengine
walio wahitaji. Jaribu kuwa mkarimu kwa Mungu utaona matunda yake!
Ewe ndugu
msikilizaji, bado tunaendelea na sehemu ya barua kwa Waebrania ambayo leo yatufundisha
kwa msisitizo tofauti kati ya kuhani mkuu wa kweli yaani Yesu Kristu na makuhani wengine.
Yesu Kristu anatolea sadaka yake si katika madhabahu yaliyotengenezwa kwa mawe bali
ukuhani wake ni wa madhabahu ya mbinguni ambayo hayakujengwa kwa mikono ya wanadamu.
Kuhani Mkuu Yesu Kristu hutolea sadaka mara moja na hutosheleza maisha yote
kwa kuondoa dhambi na kutakasa mioyo ya watu, tofauti na sadaka za makuhani wa Agano
la Kale ambazo hazikumaliza shughuli ya kuwatakasa watu, kumbe iliwapasa kurudia kila
mwaka! Basi mwaliko ni kwetu ni kumfuasa Bwana kwa kushiriki sadaka ya Misa kwa ajili
ya wokovu wetu.
Katika Injili, Mtakatifu Marko akinukuu mafundisho ya Bwana
anakazia kujitoa bila kujibakiza kama yule mama mjane aliyetoa sadaka senti mbili
ambazo ilikuwa ndiyo hazina yake! Anatoa yote bila kuogopa kwa maana analo tumaini
katika Bwana ambaye ni mgawaji wa mapaji yote. Mjane huyu ni kinyume na watu wengine
ambao hutoa ziada na si mali hasa inayotoka katika mioyo yao! Mpendwa yafaa kujitazama
moyoni wapi ulipo katika makundi haya mawili! Kama uko katika kundi la mjane basi
unayo heri ya milele na uishikilie kwa furaha maana ni zawadi toka kwa Bwana.
Basi
mpendwa ndugu unayetafakari nami, jaribu kujikuza katika sala ukiomba fadhila ya ukarimu
katika maisha yako. Kula, ishi, cheka na zungumza na wengine kwa furaha daima. Tumsifu
Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.