Kanisa kumtangaza mtumishi wa Mungu Maria Luisa Prosperi kuwa Mwenyeheri
Mtumishi wa Mungu Maria Luisa Prosperi alizaliwa tarehe 19 Agosti 1799, huko Folignano,
Kaskazini Mashariki mwa Italia, akajiunga na Monasteri ya Santa Lucia in Trevi, hapo
tarehe 4 Mei 1820 na kupewa jina la Maria Luisa Angelica wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Kwa mfano wa maisha yake matakatifu, alichaguliwa kuwa Mama mkuu wa Monasteri
tangu tarehe Mosi Oktoba 1837, kwa vipindi vinne mfululizo, hadi mauti yalipomfika
hapo tarehe 12 Septemba 1847 baada ya kuugua kwa muda mrefu, huku akiyapokea mateso
na mahangaiko yake kwa imani na matumaini; anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri
Jumamosi tarehe 10 Novemba, 2012 Jimboni Spoletto, Italia.
Tukio hili la kihistoria
katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linafuatia tukio jingine la aina hii la Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kumtangaza Mtakatifu Ildegarda wa Bingen, kuwa
Mwalimu wa Kanisa. Watakatifu hawa ni mfano na kielelezo cha kuigwa katika maisha
na utume wa Kanisa, wakati huu Mama Kanisa anapojitahidi kukuza na kuendeleza ari
na moto wa Uinjilishaji Mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Ni mchango unaotolewa
na Familia ya Shirika la Wabenediktini, kwa ajili ya utamaduni na utakatifu wa maisha
ya Kanisa.
Ni maneno ya Kardinali Angelo Amato, Rais wa Baraza la Kipapa lenye
dhamana ya kuwatangaza wenyeheri na watakatifu, anapoelezea wasifu wa Mtumishi wa
Mungu Maria Luisa Prosperi. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika barua
yake ya kichungaji, anamwelezea mtumishi huyu wa Mungu kuwa kweli ni mtawa aliyekuwa
na Ibada ya pekee katika kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kukumbatia Fumbo la Msalaba,
kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaokomboa.
Ni mtawa aliyebahatika
kuwa na karama mbali mbali alizozitumia kwa ajili ya maisha na ustawi wa Shirika lake
na Kanisa kwa ujumla. Ni mwamini aliyekuwa na imani hai ambayo kamwe haikuweza kuterereka
hata wakati wa ugonjwa wake. Ni imani iliyokuwa inabubujika kama zawadi safi kutoka
kwa Roho Mtakatifu, ikaugusa moyo wake ambao ulisheheni upendo wa Kimungu kwa jirani
zake, kiasi cha kuutolea ushuhuda makini na wenye nguvu na mvuto wa pekee. Ni mtawa
aliyekuwa na kiu ya kutaka kuonana na Mwenyezi Mungu, asili ya imani yake.
Kardinali
Angelo Amato anasema, leo hii Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, linawahitaji
waamini walei, watawa na makleri waweze kushuhudia imani yao, katika hali ya amani
na utulivu wa ndani hata wakati wanapokumbana na dhoruba katika maisha yao.