Vatican na Burundi kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Burundi
Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Burundi kwa niaba ya ujumbe wa
Vatican ameweka sahihi kwenye Mkataba wa Ushirikiano kati ya Vatican na Burundi, kwa
ajili ya mafao ya nchi hizi mbili. Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa
kimataifa Laurent Kavakure alitia sahihi kwa niaba ya Serikali ya Burundi, tukio ambalo
limehudhuriwa na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Mkataba huu unapania kuendeleza
na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia uliofikiwa kati ya Vatican na Burundi kwa takribani
miaka hamsini iliyopita. Mkataba pamoja na mambo mengine, unatoa uhakika wa kisheria
kwa Kanisa katika masuala mbali mbali, yakiwemo: ndoa zinazofungwa ndani ya Kanisa
Katoliki, maeneo ya Ibada na sala; Taasisi za elimu, afya na maendeleo endelevu; ufundishaji
wa dini shuleni, huduma za kijamii, huduma za maisha ya kiroho kwenye vikosi vya ulinzi
na usalama, magereza na hospitali. Mktaba huu utaanza kutumika pale utakaporidhiwa
na pande hizi mbili.