2012-11-08 15:25:56

Ujumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Deepval kwa Mwaka 2012


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetuma ujumbe na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kihindu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Deepval, ujumbe ambao kwa Mwaka 2012 unaongozwa na kauli mbiu "Wakristo na Wahindu wawaandae Vijana wa kizazi kipya ili waweze kuwa ni wajenzi wa amani".

Katika ujumbe huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema kwamba, mwanadamu nyakati hizi anakabiliwa na nguvu hasi zinazotishia amani na maelewano kati ya watu, ndiyo maana wanaona inafaa sana kwa waamini wa dini ya Kihindu na Kikristo kushikamana kwa pamoja ili kusaidia majiundo ya vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, waweze kuwa ni wajenzi wa amani.

Ikumbukwe kwamba, amani si kutokuwepo kwa kinzani, migogoro wala vita, lakini ni matunda ya upendo. Wadau mbali mbali wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya amani, kama kiini cha malezi ya vijana wa kizazi kipya, kwa ajili ya mafao ya wengi. Ili amani hii iweze kuwa dumifu, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, inajengeka katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuelimishwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Wadau mbali mbali wanapotekeleza wajibu na dhamana hii, wanapaswa kukazia kwamba, tofauti za kidini zinazojitokeza miongoni mwa wananchi ni utajiri mkubwa ambao wanapaswa kuulinda na kuutunza badala ya kuonekana kana kwamba, ni jambo la hatari.

Ikumbukwe kwamba, Familia ni shule ya kwanza ya amani na wazazi ni walezi wa kwanza wa amani, dhamana inayojionesha kwa njia ya mifano bora ya maisha na mafundisho yao; ni watu wenye dhamana ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii, zitakazoiwezesha Jamii kuweza: kuthaminiana, kuheshimiana, kufahamiana, kusikilizana, kushirikishana, kusaidiana na kusameheana.

Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali ambapo vijana wa kizazi kipya wanashirikishana, wanasoma na kufanya kazi kwa pamoja kutoka katika dini na tamaduni tofauti tofauti, hivyo basi, walimu na walezi katika majiundo yao wanadhama kubwa ya kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa inaheshimu, inalinda na kudumisha utu na heshima ya mwanadamu; kwa kukazia urafiki, haki, amani, ushirikiano na maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Tunu msingi za kimaadili na kiroho hazina budi kuwa ni nguzo thabiti katika utoaji wa elimu pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwa na mang'amuzi ya kina kuhusu siasa na sera ambazo zinaweza kusababisha kinzani na migawanyiko ndani ya Jamii. Serikali na viongozi mbali mbali katika maisha ya Kijamii, Kisiasa na Kitamaduni pamoja na sekta nyingine za maisha, wanao wajibu na dhamana wanayopaswa kutekeleza katika kuimarisha elimu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Viongozi wa dini kutokana na dhamana yao ya maisha ya kiroho na kimaadili wanapaswa kuendelea kuwahimiza vijana kutembea katika njia ya amani, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni wajenzi wa amani. Njia za mawasiliano ya Jamii zinamchango wake katika mchakato mzima wa kumuunda kijana wa kizazi kipya katika mawazo, vionjo na matendo yake.

Hivyo basi, wadau wa sekta ya mawasiliano ya jamii hawana budi kuhakikisha kwamba, wanasaidia kutoa mawazo yatakayokoleza mifano bora ya maisha, kwa kuwajibika barabara wanapotumia uhuru wao katika shughuli za upashanaji habari sanjari na kuhakikisha kwamba, wanajikita katika ujenzi wa utamaduni wa amani. Kwa njia hii, Jamii itaweza kujenga utamaduni wa udugu na mshikamano, kwa kutambua na kumheshimu kila mtu.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linahitimisha ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Deepvali kwa Mwaka 2012 kwa kusema kwamba, kila mtu anawajibika kutafuta na kujishikamanisha na tunu msingi za kimaadili na kidini, ili kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa kweli ni wajenzi wa amani. Ujumbe huu umetolewa na Kardinali Jean Lous Tauran, Rais pamoja na Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini.







All the contents on this site are copyrighted ©.