"Mwenyezi Mungu asili ya maisha, akuongoze katika haki na amani Rais Obama"
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, amemtumia salam
za pongezi na matashi mema Rais Barack Obama wa Marekani kutokana na kuchaguliwa kwake
kwa kishindo, kuwaongoza Wamarekani kwa kipindi kingine cha miaka minne. Anamtakia
baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu anapoendelea kutekeleza wajibu na majukumu
yake kama Rais wa Marekani.
Anasema, Baraza la Makanisa litaendelea kutolea
sala zake kwa ajili ya Rais Obama na viongozi wenzake. Akigusia kwa namna ya pekee,
mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, utakaongozwa na kauli mbiu
"Mungu asili ya maisha, anatuongoza katika haki na amani", amemwalika Rais Obama kuhakikisha
kwamba, anatumia ushawishi wake kama Rais wa Marekani katika harakati za kukuza na
kudumisha haki na amani, sehemu mbali mbali za dunia.
Ni matumaini ya Katibu
mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, Rais Obama ataendelea kuwa ni kiongozi
na mfano wa kuigwa katika Jumuiya ya Kimataifa, katika mchakato unaopania kutafuta,
kulinda na kudumisha misingi ya haki na maelewano hususan kati ya Israel na Palestina.