Matumizi ya maendeleo na sayansi katika njia za mawasiliano Maaskofu Wanapofundisha,
Ongoza na Kuwatakatifuza Watu wa Mungu
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linajipanga kikamilifu kutekeleza wajibu wake
wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu katika ulimwengu wa Utandawazi
na Maendeleo ya Sayansi na teknolojia kwa njia mpya za mawasiliano ya kijamii, kama
changamoto inayoendelea kujitokeza katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo
sanjari na Uinjilishaji Mpya.
Maaskofu wanategemea kujadili kwa kina na mapana
kuhusu matumizi ya njia za mawasiliano ya jamii, katika mkutano wao wa Mwaka utakaofanyika
kuanzia tarehe 12 hadi 15 Novemba 2012 huko Baltimore.
Kardinali Donald Wuerl,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani atazungumzia changamoto zinazojitokeza
katika Ulimwengu mamboleo na fursa zilizopo katika utekelezaji wa utume wa Maaskofu
katika kufundisha: Imani, Maadili na Utu wema. Maendeleo ya matumizi ya njia za mawasiliano
na mitandao ya kijamii imeboresha maradufu mawasiliano. Hii ni changamoto kwa Maaskofu
kujibu mara moja shutuma au pale ambapo Mafundisho Tanzu ya Kanisa yanapotoshwa au
kutafsiriwa vibaya.
Leo hii kuna sauti nyingi zinazoendelea kusikika katika
mitandao ya kijamii, Maaskofu wanajiuliza, Je, umefika wakati hata kwa wao pia kuingiza
sauti zao katika mitandao hii? Jambo hili linahitaji kwanza kabisa, Maaskofu kufafanua
dhamana na wajibu wao katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Njia za mawasiliano ya kijamii ni sawa na upanga wenye makali kuwili, kumbe, zinapaswa
kutumiwa kwa umaskini na uangalifu mkubwa zaidi, vinginevyo zinaweza kusababisha ugumu
na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kama Maaskofu mahalia.
Itakumbukwa
kwamba, hii ni fursa mpya kwa Maaskofu na viongozi wengine wa Kanisa kuweza kuwasiliana
na Waamini wao kwa haraka zaidi, ikilinganishwa na njia ambazo Mama Kanisa amekuwa
akitumia kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita.