Kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya sayansi na imani, ili
kujenga utamaduni unaomheshimu binadamu, utu na uhuru wake!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi tarehe 7 Novemba 2012 amekutana
na kuzungumza na Wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi waliokuwa wanafanya mkutano
wao wa mwaka hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi 7 Novemba 2012.
Anasema,
kuna ugumu na uwiano mkubwa katika sayansi kuhusiana na: nadharia, mbinu na mwelekeo
wake wa uandishi, mambo yanayogusa kwa namna ya pekee kabisa umoja katika masuala
ya kisayansi.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa
ya sayansi na teknolojia, mambo ambayo yamemwezesha mwanadamu kupata ufahamu mkubwa
zaidi kuhusu asili na maumbile, changamoto ya kuangalia nafasi ya mwanadamu katika
Fumbo la Uumbaji kama sehemu ya mchakato wa kutumia vyema ujuzi na maarifa yake kwa
ajili ya kutunza mazingira.
Mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu akili
na uhuru wa kuufahamu ulimwengu, changamoto ya kutumia chenzo hizi ili kupenda, kuishi
na kufanya kazi. Leo hii kuna vifaa vinavyomwezesha mwanadamu kufanya majaribio makubwa,
lakini daima akumbuke kwamba, kuna haja ya kuwa na umoja katika mchakato wa tafiti
za kisayansi ili kufahamu nguvu asilia.
Watafiti na wanasayansi waendelee
kurahisisha mafanikio haya kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, akili na hekima
ya kikristo inayopata chimbuko lake katika taalimungu na falsafa inaweza kuleta uwiano
bora zaidi kwa kutambua kwamba, mwanadamu anashiriki kwa namna ya pekee kabisa ile
kazi ya uumbaji ambayo bado inahitaji kufanyia utafiti wa kina na wanasayansi.
Falsafa
na Taalimungu iwasaidie kuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu kweli asilia na kazi ya
uumbaji, kama changamoto kwa mwanadamu kuinua macho yake, ili kutafakari ukuu wa Mungu
ambaye kwa uwamo wake, viumbe vinashiriki ukuu wa Mungu. Kwa njia hii, wanasayansi
wataendelea kufanya tafakari ya kina ili kugundua Fumbo la maisha ya mwanadamu na
ulimwengu katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema
kwamba, kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya ulimwengu wa
sayansi na imani, ili kujenga utamaduni unaomheshimu binadamu, utu na uhuru wake kwa
ajili ya mafao ya Familia ya binadamu na maendeleo endelevu hapa duniani.
Bila
mwingiliano huu anasema Baba Mtakatifu, mwanadamu atajikuta kwamba, anapoteza mwelekeo
wa akili na ukweli na hatimaye, kutekwa na vionjo; mambo ambayo ni hatari kubwa kwa
binadamu, amani na mustakabali wake.
Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake
kwa wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, kwa kuwakumbusha kwamba, Mama Kanisa
anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka
50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Ni matumaini yake kwamba, Taasisi hii
itaendelea kuchangia kuboresha na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya akili na imani
na kwamba, yuko pamoja nao katika sala.