"Endeleeni kumuenzi Marehemu Askofu Balina kwa njia ya huduma makini kwa binadamu;
kwa kudumisha, umoja, upendo na mshikamano wa dhati"
Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania anasema, wakati huu
ambapo Familia ya Mungu nchini Tanzania inaendelea kuomboleza kifo cha Askofu Aloysius
Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu
kwa sura na mfano wake, anataka binadamu amfahamu, ampende na kumtumikia. Amempatia
mwanadamu Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani.
Yote haya
yamejidhihirisha katika maisha na utume wa Marehemu Askofu Balina wa Jimbo Katoliki
Shinyanga, wakati alipokuwa anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza
na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni mwaliko wa kuendelea kumuenzi Askofu Balina kwa
kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, bila kusahau kuwahudumia jirani kwa
moyo, akili na nguvu zote, kama sehemu ya kushiriki katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa
na Kristo mwenyewe.
Mshtuko wa kifo cha Askofu Balina, kamwe kisiwe ni chanzo
cha utengano, bali Taifa la Mungu liendelee kuupokea msiba huu kwa imani, matumaini
na mapendo, daima wakijitahidi kuyatafakari mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ni
mwaliko wa kuendelea kumwombea pamoja na kuanza kuliombea Jimbo Katoliki la Shinyanga,
ili liweze kuwa tayari kumpokea Askofu mwingine, atakayeteuliwa na Mama Kanisa kuiongoza
Familia ya Mungu Jimboni humo.
Matukio yote haya yanayofumbatwa katika maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, yawasaidie waamini kuyapokea pia kwa imani na kwa kutambua kwamba,
kwa hakika Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwasikiliza na atazijibu sala zao kwa wakati
muafaka.