2012-11-07 09:22:03

Patriaki Maxim wa Kanisa la Kiothodox la Bulgaria, afariki dunia


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametuma salam za rambi rambi kwa Mheshimiwa Grigorij di Veliko Trnovo kutokana na kifo cha Patriaki Maxim wa Kanisa la Kiothodox la Bulgaria, kilichotokea mapema siku ya Jumanne, tarehe 6 Novemba, 2012 akiwa na umri wa miaka tisini na minane. Ni kiongozi ambaye kwa miaka mingi alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia ndugu zake katika Kristo.

Baba Mtakatifu anachukua fursa hii, kuwahakikishia wote walioguswa na msiba huu mzito uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala ma sadaka yake, ili Kristo mwema na mwenye huruma aweze kumpokea kwenye makao ya uzima wa milele Mtumishi wake Maxim. Baba Mtakatifu anakumbuka kwa namna ya pekee, mapokezi ambayo Marehemu Patriaki Maxim aliyatoa wakati wa hija ya kichungaji ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, Mwezi Machi 2002.

Katika kipindi cha uongozi wake, alijenga na kuimarisha uhusiano mwema na Kanisa Katoliki, changamoto ya kuendeleza ushirikiano huu, ili kwa pamoja waweze kutangaza Habari Njema ya Wokovu.







All the contents on this site are copyrighted ©.