"Msitumie vyandarua kufugia kuku na kutegea samaki"
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaelekeza
Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari za kata
nchini zinakuwa na vyumba vitatu vya maabara katika muda wa miaka miwili kuanzia Jumatatu,
Novemba 5, 2012.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake inajiandaa
kufanya ajira nyingine kubwa ya walimu katika muda mfupi ujao, ili kuzidi kukabiliana
na upungufu wa walimu katika shule mbali mbali nchini. Amewataka baadhi ya wananchi
wanaotumia vyandarua vya kupambana na ugonjwa wa malaria na vilivyogawiwa bure na
Serikali kufugia kuku kuacha mara moja tabia hiyo.
Rais Kikwete ametoa agizo
hilo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wakati alipozindua na kufungua miradi miwili
mikubwa ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Singida ambako jioni ya leo amemaliza
ziara ya siku mbili ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa huo. Miradi
hiyo miwili ni uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya
na ufunguzi wa Barabara ya Issuna-Manyoni ambayo ujenzi wake umekamilika.
Akizungumza
kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni hadi Chaya kupitia
Itigi nje kidogo ya mji wa Itigi, Mkoani Singida, Rais Kikwete amesema kuwa ni lazima
sasa kukabiliana na kumaliza matatizo yanayokabili sekta ya elimu ukiwemo ukosefu
wa maabara ambazo ndizo zitajenga msingi kwa wanafunzi wa Tanzania kuwa wanasayansi.
Rais
Kikwete amewambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uwekaji wa
jiwe hilo la msingi: “Sasa nawaagiza viongozi wenzangu- Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya, kila Mkuu wa Mkoa na kila Mkuu wa Wilaya, kusimamia ujenzi wa vyumba vitatu
vya maabara, yaani maabara ya fizikia, kemia na baiolojia kwenye kila shule ya sekondari
ya kata nchini. Kazi hii nataka ikamilike katika miaka miwili kuanzia leo. Kwa upande
wake, Serikali kuu itahangaika kutafuta vifaa vya kufunga katika vyumba hivyo.”
Akiendelea
kuwaeleza wananchi kuhusu hatua ambazo Serikali inazichukua kukabiliana na changamoto
zinazokabili elimu nchini ambayo imepanuka sana katika miaka saba iliyopita, Rais
Kikwete amesema kuwa Serikali inakamilisha taratibu za kuajiri maelfu ya walimu katika
muda mfupi ujao.
“Wakati tunaingia madarakani mwaka 2005, nchi yetu ilikuwa
inafundisha na kutoa walimu 500 kwa mwaka. Mwaka jana, idadi hiyo ilifikia walimu
12,000 na sasa tunajiandaa kugawa walimu wengine waliohitimu. Nadhani kwenye Januari,
mwakani, kila shule nchini itaongezewa walimu. Tunadhamiria kuwa katika miaka miwili
ama mitatu ijayo, tatizo la upungufu wa walimu nchini liwe ni historia,” amesema Rais
Kikwete.
Rais pia amewaeleza wananchi kuhusu jitihada zinazofanywa kukabiliana
na changamoto katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kupambana na magonjwa yanayoua
watu kwa wingi nchini ikiwamo malaria na ukimwi. Hata hivyo, Rais ameeleza kusikitishwa
kwake na tabia ya baadhi ya watu ambao wanatumia vyandarua ambavyo vimegawiwa bure
na Serikali kwa kila kaya nchini kufugia kuku ama kuvulia samaki. “Watu wetu wa ajabu
sana. Tumegawa vyandarua bure ili sote tuondokane na tatizo la malaria. Lakini nasikia
wengine wanavitumia kufugia kuku. Kweli Tanzania inahitaji ubunifu, lakini siyo ubunifu
wa namna hii wa ovyo. Tuache kutumia vyandau kufugia kuku, tuvitumie kama ilivyokusudiwa.”