Kardinali Robert Sarah kumwakilisha Papa nchini Syria kama alama ya mshikamano na
wananchi wa Syria katika kipindi hiki kigumu
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe
7 Novemba 2012 amesema kwamba, anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya machafuko
na vita vinavyoendelea kurindima nchini Syria kwa hofu kubwa, kutokana na idadi ya
waathirika kuendelea kuongezeka siku hadi siku na hivyo kusababisha mateso na mahangaiko
kwa watu wasiokuwa na hatia, ambao wengi wao tayari wameyakimbia makazi yao wakihofia
usalama wa maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema, kama alama ya mshikamano wake
na Kanisa zima kwa wananchi wa Syria pamoja na Jumuiya za Wakristo nchini Syria, alitamani
kutuma ujumbe wa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, lakini haikuwezekana.
Sasa ameamua kwamba, kuanzia tarehe 10 Novemba 2012, Kardinali Robert Sarah,
Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki atakwenda nchini
Lebanon, ambako anatarajiwa kukutana na viongozi wa Kanisa pamoja na waamini katika
ujumla wao. Atatembelea kambi za wakimbizi pamoja na kuzungumza na Mashirika ya Misaada
ya Kanisa Katoliki, ili kuratibu kwa pamoja misaada inayotolewa na Kanisa kwa ajili
ya wananchi wa Syria wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha.
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, anachukua fursa hii kuzitaka pande zote mbili zinazoendelea
kusigana pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa nchi ya Syria, kuunganisha nguvu zao,
ili amani iweze kupatikana kwa njia ya majadiliano na utulivu miongoni mwa wananchi
wa Syria, ili hatimaye, suluhu ya kisiasa iweze kupatikana.