Changamoto ya kuwa na utambulisho mpya wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika kipindi chetu cha Uinjilishaji
wa kina ambapo bado tunaendelea na uchambuzi juu ya Lineamenta ya Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji mpya. Juma lililopita tuliachana na mawazo juu ya mazingira wanayojikuta
wanafamilia ya Mungu katika kumshuhudia Kristo katika ulimwengu wa leo.
Juma hili
tuungane na Baba Mtakatifu Benedikto XVI anapoendelea kuwaasa Maaskofu wa Sinodi juu
ya namna mpya ya kuwa Kanisa katika millennia ya tatu.
Baba Mtakatifu Benedikto
XVI anabainisha kuwa mazingira ya sasa na mabadiliko makubwa kiutamaduni na kijamii
yanapelekea uhitaji na mtazamo mpya kiunjilishaji. Anataja kwa mfano, mfumo wa tangu
zamani uliozoeleka hadi leo wa kuligawa Kanisa katika nchi za Kikristu na nchi za
Missioni umepitwa na wakati wala hautoi tena picha halisi ya Kanisa la Kiulimwengu
lenye utume mmoja wa kumtangaza Kristo kwa Mataifa yote. Badala yake anapendekeza
kufanyike mabadiliko mbadala kifikra na kimtazamo katika Kanisa kwa kuzingatia maisha
ya Kanisa na Imani bila kuathiri utume msingi wa Kanisa yaani Uinjilishaji.
Kanisa
kwa namna zake zote lazima libaki daima kama Kanisa mahalia na familia ya watu wa
Mungu anasisitiza Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Hata katika mazingira magumu ya kuhujumiwa
Kanisa lazima lisipoteze ujumbe wake wa upendo wa Mungu kwa watu wake kwa kuwa daima
karibu na watoto wake katika maisha yao ya kila siku likimpeleka Kristu aliyeteseka
miongoni mwa waumini. Kanisa linaalikwa kuwaendea watu wa Mungu mahali na mazingira
yoyote walipo na kutoa majibu kwa maswali makuu ya maisha na kurudisha tumaini kwa
waliolikosa na kurudisha tena furaha ya watu hawa hata katika mahangaiko yao.
Baba
Mtakatifu kwa namna ya pekee amelitaka Kanisa katika nchi za magharibi kujikita zaidi
katika uinjilishaji mpya kwani ndio eneo hasa ambalo hapo mwanzo lilipokea imani na
kushamiri na kuwa sababu ya kuwepo kwa imani hiyo maeneo mengi ulimwenguni kupitia
makundi makubwa ya wamissionari kutoka eneo hilo. Leo hii hali imebadilika kinyume
chake.
Imani ya Kristo imepoteza ladha kwa kiwango kikubwa au imekuwa sababu
ya migogoro na chuki miongoni mwa wanajamii. Kumbe iko haja ya kuinjilisha upya ili
kufufua tena ile imani iliyopandwa hapo zamani kwa sala na sadaka kubwa. Kuna haja
ya kubuni mbinu ya kuwepo kwa Kanisa hata katika mazingira yaliyopoteza uchaji wa
Mungu na hivyo dini kukosa nafasi katika maisha ya mtu.
Baba Mtakatifu anaendelea
kubainisha zaidi tema ya Uinjilishaji Mpya akizingatia utume msingi wa Kanisa ambao
anasema utabaki vilevile miaka nenda rudi, Unjilishaji wa Mataifa yote kuwa wanafunzi
wa Yesu. Tunapozungumazia uinjilishaji mpya anasema Baba Mtakatifu inamaanisha tu
kuwa haiwezekani kwa mfano nchi za Kikristo kuendelea kuinjilisha nchi zingine zikisahau
makundi makubwa ya wasio wakristu nyumbani.
Kumbe, nyakati hizi ni zama za
kurudi nyuma na kuimarisha wale walio nyumbani. Kwa uinjilishaji mpya Kanisa linaingia
katika kipindi kipya chenye changamoto mpya ma mtindo mpya wa uinjilishaji ambapo
ujumbe unabaki ule ule kwani Kristo ni Yule Yule: Jana, Leo na hata Milele.
Uinjilishaji
mpya anendelea kubainisha Baba Mtakatifu, ni jina linalotajwa kuonesha utume wa Kanisa
katika mtindo mpya katika mazingira mapya ya sasa. Uinjilishaji mpya unaligusa Kanisa
zima linaporudi mahali lilipo na kuthathmini hali halisi ya ushuhuda wa imani miongoni
mwa watu wake bila kuangalia maeneo fulani tu ya kuinjilisha. Kanisa mahalia sasa
linaalikwa kujikita zaidi na uimarishaji wa imani nyumbani au mahali pale lilipo.
Uinjilishaji mpya unalenga kumpeleka Kristo ulimwenguni kumbe Kanisa zima
linahusika: Kanisa katika nchi za Kikristo liendelee kupambana na tatizo la uasi dini
miongoni mwa waumini wake wakati katika nchi za kimissionari, Kanisa liendelee na
utamadunisho ili mradi Imani iendelee kutoa mwanga, na mwelekeo sahihi na uzima kwa
watu wa Mungu popote pale walipo.
Mpendwa msikilizaji kufikia hapo tumefikia
mwisho wa kipindi chetu kwa siku ya leo. Tuendelee kuwa wasikivu na macho kusikiliza
na kusoma yale tunayoalikwa kuyatekeleza kutoka katika Sinodi ya Uinjilishaji Mpya.
Mungu akubariki sana, nikikuaga kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi mtayarishaji
na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.