2012-11-06 08:20:04

Mabalozi kutoka Nigeria, Australia na Colombia wawasilisha hati zao za utambulisho mjini Vatican


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu tarehe 5 Novemba, 2012 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa Nigeria, Australia na Colombia wanaoziwakilisha nchi zao hapa mjini Vatican.

Balozi Francis Chukwuemeka Okeke kutoka Nigeria, alizaliwa kunako tarehe 10 Oktoba 1952. Kitaaluma ni daktari wa binadamu na bingwa katika upasuaji. Amefanya kazi zake sehemu mbali mbali za Nigeria, Ireland, Uingereza na anamiliki kituo kikubwa cha Afya mjini Enugu, Nigeria.

Balozi John Anthony Gerald McCarthy, kutoka Australia, alizaliwa 20 Oktoba 1947. Kitaaluma ni mwanasheria, kazi ambayo ameitekeleza sehemu mbali mbali nchini mwake. Amewahi kuwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Margaret iliyoko Sydney, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sanaa Mamboleo na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kanisa Katoliki Australia kwa ajili ya Makanisa yanayoteseka. Ni mwandishi mzuri wa vitabu, makala na majarida.

Balozi Germàn Cardona Gutièrrez kutoka Colombia, alizaliwa tarehe 28 Desemba 1956. Ni kiongozi aliyebobea katika masuala ya uongozi. Amewahi kuwa Jaalimu, Gavana, Meya, Mkurugenzi katika Taasisi ya Kupambana na rushwa nchini Colombia na pia Waziri wa Usafirishaji, kazi ambayo aliifanya kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2012.







All the contents on this site are copyrighted ©.