Kumbu kumbu ya miaka 125 ya Kampeni ya Kardinali Lavigerie dhidi ya biashara haramu
ya utumwa Barani Afrika
Wamisionari wa Afrika (White Fathers) na Masista Wamisionari wa Mama yetu Malkia wa
Afrika (White Sisters) watasherehekea kumbukumbu ya miaka 125 ya kampeni ya mwanzilishi
wao, Kardinali Lavigerie Charles, ya kupambana na Biashara haramu ya Utumwa Barani
Afrika.
Kumbukumbu
hii itazinduliwa tarehe 11 Novemba 2012 katika Kanisa la Gesù, lililoko mjini Roma
kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu mkuu Michael Fitzgerald, Balozi
wa Vatican nchini Misri na itafungwa hapo tarehe 8 septemba, 2013, mjini Ouagadougou,
Burkina Faso. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya kwa mwaka huu ni: "Mimi ni mwanadamu
na hakuna chochote cha kibinadamu kilicho kigeni kwangu."
Sababu za kuadhimisha
kumbukumbu hii:
Kwanza kabisa ni kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili
ya mafanikio ya kampeni hii. Licha kufutwa kwa biashara haramu ya binadamu, lakini
bado kuna uwepo na ongezeko la aina mpya za utumwa mamboleo katika jamii nyingi duniani.
Ni vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kama ilivyokuwa wakati wa
biashara haramu ya utumwa, miaka mia moja na ishirini na mitano iliyopita.
Hii
ni changamoto ya kuimarisha tafakari na dhamira zetu kuhusu kusimama kidete kulinda
na kutetea haki na amani, hasa katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, tukifuata
nyayo za Mwanzilishi wetu. Zaidi ya hayo, tutafanya kumbukumbu hii pamoja na Kanisa
zima ambalo lilimkabidhi Kardinali Lavigerie utume huu, kupitia kwa Baba Mtakatifu
Leo XIII hapo tarehe 21 Mei 1888.
Kampeni ya Kardinali Lavigerie ya kupambana
na utumwa Barani Afrika Kabla ya uzinduzi wa kampeni hii:
Kardinali Lavigerie
alikutana na waathirika wa mauaji ya kinyama nchini Lebanon na Syria yaliyotokea
kunako mwaka 1860. Alifanikiwa kukutana na waathirika wa baa la njaa nchini Algeria
kunako mwaka 1868. Aliguswa kwa namna ya pekee na waathirika wa biashara ya utumwa
iliyokuwa inatendeka Kusini mwa Algeria, kwa mfano Laghouat na Ouargla. Kuanzia mwaka
1872 na kuendelea na Afrika ya Masharaki kupitia kwa shuhuda za wamisionari wake,
kuanzia mwaka 1879 na kuendelea.
Baada ya kusikia kwa kina na mapana, kuna
haja ya kutekeleza mambo yafuatayo kwa ajili ya kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wawaonjeshe jirani zao moyo
wa huruma kwa njia ya huduma kwa waathirika. Kuna haja ya kuendeleza juhudi za kuwakomboa
watu kutoka katika utumwa mamboleo, hasa miongoni mwa watoto, wanawake na vijana kwa
kutoa elimu makini.
Neno huruma lilikuwa ni kati ya maneno aliyoyatumia kwenye
Nembo yake. Ni Kiongozi aliyeguswa na mahangaiko ya watu kiasi kwamba, utume wake
mzima, ulikereka na vitendo vya kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Kardinali Lavigerie
alitambua kwamba, huruma peke yake ilikuwa haitoshi kuliokoa Bara la Afrika kutoka
katika biashara haramu ya utumwa. Ndiyo maana kwa busara ya kichungaji alipenda kuunganisha
upendo na huduma kama sehemu ya mchakato wa kupambana na hatimaye, kung’oa kabisa
mizizi iliyopelekea uwepo wa biashara haramu ya utumwa.
2. Kampeni yake:
1888-1892
Katika mpango wake wa 'Uinjilishaji wa Afrika" miaka kumi kabla
ya kampeni hii, Lavigerie alikuwa tayari amependekeza "kukomesha biashara ya watumwa"
kama moja ya njia za uinjilishaji huo. Alitumia fursa ya kukomeshwa kwa biashara ya
utumwa nchini Brazil kwa kumwomba Baba Mtakatifu Leo XIII, ashutumu vikali biashara
haramu ya watumwa Barani Afrika, katika Waraka wake wa kichungaji ”In Plurimis” aliouandika
kwa ajili ya tukio hilo hapo tarehe 5, Mei, 1888. Baba Mtakatifu akamkabidhi dhamana
ya kupambana na biashara haramu ya utumwa Barani Ulaya, kuanzia tarehe 21 Mei, 1888.
Lengo
la kampeni hii, lilikuwa ni kukomeshwa biashara ya watumwa Kusini mwa Jangwa na Sahara.
Ili kufanikiwa ilimbidi kuwajengea watu uwezo kwa njia ya Kampeni kwa watu wanaoishi
Barani Ulaya kwa ajili ya watu wa Afrika. Aliwataka wananchi wa Bara la Ulaya kuzishirikisha
Serikali zao kwa kuonesha madhara ya biashara haramu ya utumwa, ili kuchukua hatua
za kisheria dhidi ya nyanyaso hizi kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kuhakikisha
kwamba, sheria hizi baada ya kutungwa, zinatekelezwa.
Kardinali Lavigerie
alipata msukumo wa pekee kupambana na biashara haramu ya binadamu kwa kuzingatia sheria
asilia na sheria za Kimungu, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kupambana na
madhulumu haya, akisukumwa na ubinadamu na uelewa wake katika masuala ya kidini. Utumwa
unapingana na kweli za Kiinjili, sheria asilia na sheria za Kimungu. Haya ni masuala
yanayogusa imani, akili, haki, heshima, upendo na uhuru wa mtu.
Alithamini
ubinadamu wake na kwake, hakuna chochote cha kibinadamu ambacho kilikuwa ni kigeni
kwake. Uonevu huu ulikuwa unatia kasoro katika asili ya maisha yake. Angependa watu
kumpatia uhuru, heshima kwa kuthamini pia utakatifu wa maisha ya Familia.
Alitamani
kuona kwamba, watu waliokombolewa kutoka utumwani wanarejeshewa furaha, thamani ya
familia, heshima na uhuru wao. Kardinali Lavigerie anatambua Sheria ya kiungu kwamba:
Mungu ni Muumba na Mkombozi wa watu wote. Binadamu wameumbwa kwa mfano wake na sura
yake, huu ndio msingi wa heshima, utu na haki ya binadamu inayokiukwa na biashara
haramu ya utumwa.
Mbinu alizotumia katika kufanikisha kampeni yake ni pamoja
na mikutano ya kitaifa na kimataifa. Akaandika: barua, makala na taarifa kwa ajili
ya kusambaza kwenye vyombo vya habari, ili kuwafikia watu wengi zaidi. Alisimamia
uanzishwaji wa vyama vya kupambana na biashara haramu ya utumwa Barani Ulaya. Alianzisha
huduma za kijamii hasa elimu na afya kwa afya kwa watoto waliokombolewa kutoka utumwani.
Aliendelea kutegemea sana Sala kama moja ya nyenzo muhimu katika Kampeni hii.
Kwake, Uinjilishaji Barani Afrika ulikuwa unakwenda sanjari na utoaji wa elimu pamoja
na kuwashirikisha wanawake katika kampeni hii, jambo ambalo halikuwa rahisi sana kwa
wakati huo, kutokana na mfumo dume kuendelea kutawala.
3. UTUMWA MAMBOLEO
Kwa
ujumla, tunaweza tukasema kwamba, kitu au jambo lolote linalodhalilisha na kukiuka:
heshima, hadhi na haki msingi za binadamu ni utumwa, bila kujali: jinsia, rangi, imani
au dini ya mtu. Orodha ya utumwa mamboleo ni kubwa sana, kwani inazihusisha pia taasisi
ambazo zinajikuta zinawatumbukiza watu katika utumwa: hizi ni pamoja na kazi za suluba,
madeni makubwa, biashara haramu ya binadamu, utumwa ndani ya familia pamoja na kambi
za kazi za suluba Na ndani ya makundi hayo tunaweza kuorodhesa vitendo vya utumwa
kama vile ajira ya watoto wadogo, biashara haramu ya ngono pamoja na ndoa za shuruti.
4. Mapambano na aina mpya za utumwa: Msukumo kutoka Kardinali Lavigerie
Tunapenda
kufuata nyayo za Kardinali Lavigerie katika kupambana na utumwa mamboleo katika mikakati
na mipango yetu ya kichungaji, kwa kuzingatia kwanza kabisa maisha ya sala kama chemchemi
ya kuzuia, ili hatimaye kung’oa mizizi ya biashara haramu ya utumwa; kuweka mikakati
ya kuzuia kwa kuwawezesha watu: kiakili na kiimani. Ni jukumu la wadau mbali mbali
kuhakikisha kuna utekelezaji na sheria zinatekelezeka.
Waathirika wapewe ulinzi
pamoja na kujengewa uwezo wa kujitegemea, ili kuheshimu hadhi na utu wao kama binadamu.
Ili kufanikisha mapambano haya anasema kardinali Lavigerie, kuna haja ya kujenga umoja
na mshikamano wa dhati na wadau mbali mbali, kwani vitendo hivi ni kinyume kabisa
cha utu na heshima ya binadamu; ni kinyume cha sheria asili inayowagusa watu wote
bila ubaguzi wowote ule. Mshikamano huu unajikita si tu katika mambo ya imani, akili,
bali unagusa kwa namna ya pekee, haki, heshima, upendo na uhuru wa mtu.
5. Dhamira
zakuzingatia wakati wa mwaka huu (2012-2013)
Katika mwaka huu 2012 hadi 2013:
Kumbukumbu na tafakari yetu itazingatia masuala yafuatayo: Utumwa wa watoto, Haki
za Binadamu Barani Afrika, Biashara haramu ya binadamu, Upokonyaji wa ardhi, Uhamiaji
na Umaskini.
6. Kalenda
Maadhimisho haya yatafuata Kalenda ya Shirika
katika Makanisa mahalia, yaani kadiri ya mipango ya Kanda za Wamissionari wa Afrika
na Masista Wamissionari wa Mama Yetu Malkia wa Afrika sanjari na kuihusisha sekta
ya watu binafsi pamoja na waamini walei na vyama vya kitume. Tutakuwa na siku tatu
tu za kuzingatiwa na wanachama wote wa Wamisionari wa Afrika na Masista Wamisionari
wa Mama yetu Malkia wa Afrika. Siku hizi ni:
11 Novemba 2012: Missa Takatifu
ya uzinduzi wa shughuli za mwaka. Mjini Roma tukio hili litaambatana na:Maonesho ya
picha za Kampeni ya Kardinali Lavigerie pamoja na picha zinazoonesha utumwa mamboleo.
Kutafanyika mkutano kuhusu Kampeni hii pamoja na kuonesha madhara ya biashara haramu
ya binadamu.
Tarehe 30 Aprili 2013: Sikukuu ya Mama yetu wa Afrika:Itakuwa
ni Siku ya Mafungo itakayoongozwa na dhamiri juu ya ukombozi. Tarehe 8 Septemba, 2013:
Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria. Maadhimisho ya hitimisho la Kumbukumbu ya miaka
mia moja na ishirini na mitano tangu kampeni ya kupinga biashara haramu ya binadamu
ilipoanzishwa yatakuwa huko mjini Ouagadougou, Burkina Faso.