Kongamano la Shirikisho la Wasalesiani kufanyika mjini Roma kuanzia tarehe 8 hadi
11 Novemba 2012
Shirikisho la Wasalesiani Kimataifa, lililoanzishwa kunako mwaka 1876 na Mtakatifu
Yohane Bosco, linalowajumuisha: waamini walei, watawa na makleri, litakuwa na Kongamano
la Kimataifa, kuanzia tarehe 8 hadi 11 Novemba 2012 hapa mjini Roma.
Kongamano
hili linawashirikisha wajumbe mia tatu kutoka katika ngazi mbali mbali: kitaifa na
kimataifa. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu: Mradi wa maisha ya kitume: kwa njia
ya uaminifu kwa karama ya Mtakatifu Yohane Bosco. Lengo ni kutaka kupembua na hatimaye,
kupitisha Katiba ambayo itakuwa ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao ndani
ya Kanisa, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Wajumbe watapata fursa
ya kumchagua Mratibu mkuu, atakayeongoza Shirikisho hili kwa muda wa miaka sita.
Shirikisho
hili limekuwa ni kielelezo cha ushuhuda makini unaotolewa na wanachama wake katika
medani mbali mbali za maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Lakini wanachama
ambao wanatambulikana kutokana na mchango wao makini katika sekta ya elimu, maendeleo
jamii, siasa na utume wa Uinjilishaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.