2012-11-06 10:10:59

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lampongeza Papa Tawadros kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa la Kikoptic nchini Misri


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, ametuma salam za matashi mema na pongezi kwa Askofu Anba Tawadros II kwa kuchaguliwa kwake kuwa Papa wa Kanisa la Kikoptik la Kiothodox la Misri hapo tarehe 5 Novemba 2012. Anampongeza kwa kuchaguliwa kuliongoza Kanisa la Kikoptik, lenye idadi kubwa ya waamini katika Nchi za Kiarabu.

Dr. Tveit katika salam zake anabainisha mchango mkubwa ambao umeendelea kutolewa na Papa Tawadros katika mchakato unaopania kujenga na kudumisha majadiliano ya Kikumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo nchini Misri. Ni matumaini yake kwamba, anapotekeleza utume wake kama Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikoptik, atadumisha zaidi uhuru, usawa, haki na amani na kwamba, sauti yao ya Kinabii itaendelea kusikika, kama sehemu ya mwendelezo wa historia na mchango wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri.

Dr. Tveit anasema kwamba, kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo na yale ya kidini na wafuasi wa dini ya Kiislam; daima wakipania kutafuta mafao ya wengi, amani na utulivu. Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, Papa AnbaTawadros ataimarisha umoja na mshikamano uliokuwepo wakati wa uongozi wa Papa Shenouda wa tatu.

Papa Tawadros anakuwa ni Patriaki wa mia moja na kumi na nane wa Kanisa la Kikoptik la Kiothodox, anayechukua nafasi ya Hayati Papa Shenouda wa tatu. aliyefariki dunia mwezi Machi 2012. Papa Tawadros alizaliwa Mwezi Novemba 1952, kitaaluma ni Mwanataalimungu mahiri na Mfamasia.







All the contents on this site are copyrighted ©.