Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaomboleza kifo cha Askofu Aloysius Balina
wa Jimbo Katoliki Shinyanga
Askofu Aloysius A. Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga amefariki dunia tarehe 6 Novemba
2012, akiwa anapata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza, baada ya kusumbuliwa
na ugonjwa wa Saratani kwa muda mrefu. Marehemu Askofu Balina alizaliwa tarehe 21
Juni 1945, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, alipadrishwa tarehe 27 Juni
1971.
Licha ya kufanya shughuli mbali mbali za kitume Jimboni Shinyanga, Marehemu
Askofu Balina aliwahi kuwa Gombera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Pio wa kumi, Makoko,
Jimbo Katoliki la Musoma. Aliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kuwa Askofu
na hatimaye, kumwekwa wakfu hapo tarehe 6 Januari 1985 mjini Roma, akiwa ni Askofu
wa kwanza wa Jimbo Katoliki Geita na kusimikwa rasmi hapo tarehe 10 Machi 1985.
Kunako
tarehe 23 Septemba 1997 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alimwamisha Askofu Balina
kutoka Jimbo Katoliki la Geita na kumpeleka Jimbo Katoliki la Shinyanga na kusimikwa
rasmi kama Askofu wa tatu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, hapo tarehe 16 Novemba 1997.
Akizungumza
na Radio Vatican, Mheshimiwa Padre Athony Makunde, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania anasema, Baraza la Maaskofu limepokea habari hizi kwa mshtuko mkubwa,
kwa imani na matumaini katika maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Kanisa linapoadhimisha
Mwaka wa Imani. Kanisa Katoliki Tanzania lilikuwa bado linahitaji mchango wake mkubwa
katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Marehemu Askofu Aloysius
Balina kwa muda mrefu alikuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania. Matunda ya uongozi wake yanajidhihirisha kwa namna ya pekee, kutokana
na maboresho ya huduma mbali mbali zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
iliyoko Jimbo Katoliki la Mwanza. Juhudi zake zimepelekea hata kuanzishwa kwa Chuo
Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Mwambata, Bugando, Mwanza, CUHAS.