Vitendo vya kigaidi bado vinajitokeza nchini Kenya
Kwa siku za hivi karibuni Kenya imeendelea kuwa ni uwanja wa vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha
amani, utulivu na usalama wa nchi. Jumapili iliyopita, mtu mmoja alipoteza maisha
na wengine kumi na moja wamejeruhiwa vibaya baada ya kulipukiwa na bomu lililotupwa
karibu na Kanisa eneo la Garissa linalopakana na Somalia. Baadhi ya wachunguzi wa
mambo wanabainisha kwamba, tukio hili linavionjo vya kisiasa zaidi kuliko kinzani
za kidini.
Tangu Kenya ilipoamua kulivalia njuga tatizo la vitendo vya kigaidi
vilivyokuwa vinafanywa na Kikundi cha Al Shebaab kutoka Somalia, imejikuta mara nyingi
ikitikiswa kwa vitendo vya kigaidi. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Julai, 2012, Makanisa
mawili yalilipuliwa katika eneo la Garissa na kusababisha watu 18 kupoteza maisha
yao. Matukio ya kigaidi hata kwa siku za hivi karibuni yamejionesha Nairobi.