2012-11-05 09:57:38

Uchumi wa Tanzania unacharuka, lakini wakulima vijijini wamesahaulika!


Taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kuboreka siku hadi siku, lakini kwa bahati mbaya, wakulima vijijini wamesahaulika katika mchakato huu, ingawa kilimo kimekuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

Benki ya Dunia inabainisha kwamba, uchumi wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2013 na 2014 unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7. Sekta zinazoongoza kwa sasa ni madini, taasisi za fedha na mawasiliano. Matumaini ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni kutokana na kugunduliwa kwa gesi asilia na mafuta nchini Tanzania. Uzalishaji wa nishati hii unaweza kuanza katika kipindi cha miaka saba hadi kumi kuanzia sasa.

Sera ya Kilimo Kwanza, inayopewa msukumo wa pekee na Serikali ya Tanzania, inaweza kuleta mabadiliko katika maisha ya wakulima wengi vijijini, ili kuendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.