Wakenya simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano
wakati wa uchaguzi mkuu 2013
Askofu mkuu Alain Paul Lebeaupin, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Kenya ambaye
hivi karibuni aliteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuwa Balozi wa
Vatican kwenye Umoja wa Nchi za Ulaya wenye makao yake makuu mjini Brussels, Ubelgiji,
anawataka wananchi wa Kenya kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika
nchini humo hapo tahere 4 Machi, unakuwa, huru, wa haki kwa kuzingatia pia misingi
ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Askofu mkuu Lebeaupin anawataka wananchi
wa Kenya kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, madhara makubwa yaliyojitokeza kwa
watu na mali zao mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika
mwaka 2007 hayajirudii tena katika historia ya wananchi wa Kenya.
Askofu mkuu
Lebeaupin anasema, alifika nchini Kenya kunako mwaka 2005 na katika kipindi chote
hiki ameshuhudia mabadiliko makubwa katika maisha ya watu wa Kenya. Anakumbuka kwa
namna ya pekee, Kura ya Maoni iliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
ambayo imesaidia kujenga umoja wa kitaifa, ingawa bado inakabiliwa na changamoto nyingi.
Askofu mkuu Lebeaupin ameyasema hayo katika dhifa iliyoandaliwa kwa niaba
yake, hivi karibuni kwa ajili ya kumuaga, baada ya kuhitimisha utume wake nchini Kenya
kama Balozi wa Vatican. Anasema kwamba, anaondoka nchini Kenya akiwa na kumbu kumbu
hai kabisa ya maisha na utume wake nchini humo, baada ya kuihudumia Familia ya Mungu
kwa takribani miaka saba.
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya, amemtakia kheri na baraka pamoja na kupona haraka kutokana na ajali
iliyomfika Mwezi Mei, 2012, akiwa mjini Roma. Amempongeza kwa utume wake uliopelekea
utekelezaji wa mikakati mingi ya maendeleo: kiroho na kimwili kwa ajili ya maisha
ya Kanisa na ustawi wa wananchi wa Kenya katika ujumla wao.