2012-11-03 11:17:54

Vitisho na woga ni sumu hatari ya ukweli dhidi ya mchakato unaopania kujenga na kudumisha mafao ya wengi na haki jamii!


Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville, imeandika ujumbe wa mshikamano na Askofu Michele Russo, ambaye hapo tarehe 30 Septemba 2012 alifukuzwa nchini Ciad, baada ya kukemea matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa nchi kutokana na mafuta, wakati wa mahubiri yake Kanisani. Tume ya haki na amani inasema kwamba, huu ni uvunjifu wa haki msingi na uhuru wa mtu kujieleza; ni kwazo katika mchakato mzima unaopania kukuza na kudumisha majadiliano kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Ciad.

Serikali ya Ciad ilimfukuza Askofu Michele Russo nchini humo kwa sababu alifanya vitendo "kinyume cha wajibu wake wa kiroho katika Jamii". Tume ya haki na amani inabaianaisha kwamba, ni wajibu na dhamana ya Kanisa, kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi; pamoja na kupambana na baa la umaskini unaokwamisha maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazaville linabainisha kwamba, kila mwamini anayo haki ya kujieleza kadiri ya Katiba ya nchi, bila kujali msimamo wake wa kiimani, kiitikadi, kijamii wala kiuchumi. Maaskofu wamesikitishwa sana na uamuzi uliochukuliwa na Serikali ya Ciad cha kumfukuza Askofu Michele Russo kutoka nchini mwao. Hali iliyobainishwa na Askofu Russo ingekuwa ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha majadiliano yanayopania kuleta maboresho ya kweli katika maisha ya wananchi wa Ciad.

Askofu Russo ni sauti ya kinabii inayoonesha mateso na mahangaiko ya wananchi wa Ciad kutokana na baa la umaskini, ingawa kuna rasilimali na utajiri mkubwa unaoendelea kuwanufaisha watu wachache katika Jamii. Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville inabainisha kwamba, vitisho na woga ni sumu ya maendeleo, ambayo kamwe haitaweza kuinyamazisha sauti ya ukweli wala kulegeza kamba ya mapambano dhidi ya ukosefu wa haki pamoja na kupania kujenga na kudumisha amani.

NI matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville kwamba, siku moja wataweza kukutana ili kuanza mchakato wa upatanaisho, ili hatimaye, Ciad iweze kujenga na kuimarisha msingi wa haki jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.