Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zake kwa waamini
Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji mpya anabainisha
kwamba, Mwaka wa Imani uliofunguliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi ni sita mjini
Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya
Uinjilishaji mpya sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka hamsini tangu Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican ulipozinduliwa bila kusahau kumbu kumbu ya miaka ishirini
tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekesimu
Mpya ya Kanisa Katoliki, ni matukio muhimu sana katika kuamsha na kukoleza imani miongoni
mwa waamini.
Hii ni changamoto
ya kufanya tafakari ya kina, kuhusu maisha na utume wa Kanisa kwa takribani miaka
hamsini iliyopita, bila kuukimbia ukweli na changamoto zinazoendelea kulikabili Kanisa
katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo; yaani tabia ya ukanimungu na watu
kupenda mno malimwengu. Wakristo wanapaswa kusimama kidete kuifahamu, kuiungama, kuitetea
na kuilinda imani yao. Matukio haya yalenge kukoleza imani kwa Kristo na Kanisa lake,
kama njia ya kujipatia wokovu.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili
ya Uinjilishaji mpya ni fursa kubwa kwa Mababa wa Sinodi kuweza kupembua changamoto,
matatizo na matumaini ya Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mababa wa Sinodi wanatafakari
kwa kina, jinsi ambavyo Mama Kanisa anaweza kurithisha, kushirikisha na kuimwilisha
imani hiyo katika uhalisia wa maisha ya watoto wake waliotawanyike sehemu mbali mbali
za dunia. Ni fursa muhimu kwa Kanisa katika kupambanua njia na mikakati ya kichungaji
itakayochukuliwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa miaka ijayo kuanzia
sasa.
Askofu mkuu Fisichella anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa
ajili ya Uinjilishaji mpya yanakwenda sanjari na Mwaka wa Imani, kwani kwa pamoja,
matukio haya makuu, yanafumbatwa katika kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Sinodi
juu ya Uinjilishaji mpya, yaani Uinjilishaji mpya ni nyenzo ya utangazaji wa imani
ya Kikristo.
Ni mwaka ambao Baba Mtakatifu anapania kuona kwamba, waamini
wanaifahamu, iungama na kuishuhudia imani yao katika maisha na vipaumbele vyao, ili
hatimaye, jirani zao waweze pia kuonja uzuri wa Injili unaojionesha katika maisha
ya Wakristo. Ni mwaliko kwa waamini hawa kukuza na kuimarisha uhusiano wao wa dhati
na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume
wa Kanisa, dhamana ambayo Mama Kanisa amejitwalia kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita.
Mama Kanisa anadhamana endelevu ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho
ya dunia, kama njia ya kushiriki ujumbe ambao Kristo mwenyewe aliupokea kutoka kwa
Baba yake wa mbinguni. Uinjilishaji Mpya ni dhana inayopania kuwawezesha waamini kukabiliana
na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao hapa duniani, katika ngazi ya
mtu binafsi na jumuiya ya waamini, wanapojitahidi kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu, limbuko lao walio lala katika mauti.
Uinjilishaji
mpya unapania kutoa fursa kwa waamini kuonesha imani yao katika maadhimisho ya Ibada
na Liturujia mbali mbali zinazoandaliwa na Mama Kanisa, Ushuhuda wa imani hiyo katika
uhalisia wa maisha ya waamini kwa njia ya Injili ya upendo.
Mababa wa Sinodi
wametafakari kwa kina: matatizo, changamoto na fursa za Uinjilishaji mpya katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo kama vile: tabia ya ukanimungu, tatizo la wakimbizi,
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, hali ya uchumi kimataifa, kumong’onyoka
kwa misingi ya maadili na utu wema; njia za mawasiliano ya jamii na changamoto na
fursa zake.
Yote haya yanaweza kupata ufanisi mkubwa kwa waamini wenye kujibidisha
kumwilisha ndani mwao tunu msingi za maisha ya Kikristo na Mapokeo yake. Waamini hawana
budi kutubu na kuongoka, kama njia ya kumkaribisha Kristo aweze kufanya hija ya maisha
pamoja nao! Mama Kanisa hana budi kuendeleza juhudi za utamadunisho, changamoto iliyotolewa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kweli, imani iweze kumwilishwa.
Jambo la msingi anasema Askofu mkuu Fisichella ni toba na wongofu wa ndani;
ushuhuda wa imani unaojionesha katika vipaumbele vya maisha ya mwamini, kwa kutambua
kwamba, Mama Kanisa anawaalika kuishi kwa namna ya pekee, utume wao kama sehemu ya
historia ya wokovu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati.
Katika kipindi
cha miaka kumi iliyopita, Mama Kanisa amefanikiwa kujenga mang’amuzi na uwezo mkubwa
katika azma ya Uinjilishaji, umefika wakati sasa kuhakikisha kwamba, mang’amuzi haya
yanafanyiwa kazi kwa ajili ya utume na ustawi wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.
Juhudi hizi zianzie kwa namna ya pekee, ndani ya mtu binafsi, familia, parokia na
vyama vya kitume, kila mwamini apanie kuonesha ushuhuda wa imani yake, kwani kila
mwamini kwa hakika ni mwinjilishaji, dhamana na wajibu aliojitwalia kwa njia ya Sakramenti
ya Ubatizo.