2012-11-03 09:22:32

Kanisa lina dhamana ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja chini ya Kristo!


Askofu mkuu Boniface Lele, Mwenyekiti wa Tume ya Majadiliano ya Kiekumene ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, anawaalika viongozi mbali mbali wa Madhehebu ya Kikristo nchini humo kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kudumisha umoja wa Kanisa mintarafu Mafundisho ya Kikristo, badala ya kuendekeza mambo yanayowagawa.

Askofu mkuu Lele ameyasema hayo hivi karibuni, wakati viongozi wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo walipofika Ofisini kwake ili kumtembelea. Kanisa Katoliki tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, limeendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, likipania kuhakikisha kwamba, wafuasi wote wa Kristo wanakuwa chini ya mchungaji wao mmoja yaani Yesu Kristo na kwa njia hii, litaweza pia kudumisha umoja kati ya watu mbali mbali.

Kanisa Katoliki kupitia Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja wa Kikristo kwa kushirikiana na Tume za Kiekumene za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki zimepewa dhamana ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene katika maeneo yao. Viongozi hao walikuwa na lengo pia la kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2013; kuanzia tarehe 18 hadi 25 Januari 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.