2012-11-03 08:10:39

Baba Mtakatifu atembelea na kusali kwenye Makaburi ya Mapapa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican


Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Marehemu wote, hapo tarehe 2 Novemba, 2012, majira ya jioni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alikwenda kutembelea na kusali kwa kitambo kwenye makaburi ya Mababa Watakatifu yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Baba Mtakatifu aliwaalika wale waliokuwa wameandamana naye wakati wa kutembelea makaburi hayo kuwaombea viongozi hawa wa Kanisa huruma na upendo wa Mungu, wakati huu wakiwa wamelala katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko wa uzima wa milelle. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu aliwakumbuka Mapapa ambao walijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuiongoza Familia ya Mungu, ili waweze kushiriki liturujia ya mbinguni.

Siku ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Wote imetumiwa na waamini sehemu mbali mbali za dunia, kutembelea, kusali pamoja na kusafisha makaburi, kama njia ya kuwaenzi waamini hao ambao wametangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la uzima wa milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.