2012-11-03 13:27:55

"Angalieni Fumbo la Kifo kwa jicho la imani na matumaini kwa Mungu aliyewaumba na kuwakomboa"


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe 3 Novemba 2012 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia kuanzia mwezi Novemba 2011 hadi Oktoba 2012, kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Liturujia ya kuwaombea wafu pamoja na kutembelea makaburi, imekuwa ni fursa kwa waamini kuweza kuonesha ule uhusiano uliopo kati yao na marehemu wao. Makaburi ya marehemu ni kioo cha maisha yao hapa duniani, mwaliko wa kuendeleza majadiliano kuhusu kifo ambacho kimeendelea kuleta mahangaiko makubwa katika maisha ya mwanadamu.

Makaburi anasema Baba Mtakatifu ni mahali ambapo watu wanakutana na marehemu ndugu zao, ili kuendeleza umoja ambao kifo kamwe hakiwezi kuutenganisha. Mjini Roma kwa namna ya pekee, kuna Makaburi ya zamani yanayoonesha kwa namna ya pekee, uhusiano endelevu uliopo na Ukristo tangu awali.

Mtu anapotembelea makaburi inakuwa kana kwamba, anaendeleza mawasiliano na wale ambao wametangulia mbele ya haki; watu ambao walionja furaha, huzuni, kushindwa na matumaini, kwani kifo kinamgusa kila mtu na makali yake yanabaki vile vile hata baada ya miaka nenda miaka rudi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuliangalia Fumbo la Kifo kwa Jicho la Imani na Matumaini kwa Mwenyezi; matumaini ambayo yanabubujika kutokana na kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, kiasi cha kumfungulia mwamini mlango wa maisha ya uzima wa milele ili kujenga umoja na Mwenyezi Mungu aliye hai pamoja na jirani aliowaumba na kuwakomboa. Hili ni jibu makini la matumaini kwa upendo wa Mungu unaong'ara juu ya Msalaba wa Kristo; mwaliko wa kujiunga naye ili kupata uzima wa milele.

Katika imani na sala, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea Marehemu Makardinali kumi na Maaskofu mia moja na arobaini na tatu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2011 hadi Oktoba 2012. Amewaombea marehemu wote hawa ili waweze kupata tuzo ambalo Mwenyezi Mungu amewaahidia Wahudumu wa Injili. Hawa ni watu waliojivika kwa dhati kabisa kheri za mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu.

Ni viongozi waliolihudumia Kanisa kwa uaminifu na upole hata wakati mwingine walikabiliana na magumu katika maisha na utume wao, lakini wakasimama kidete kuwalinda na kuwatetea Wanakondoo waliokabidhiwa kwao na Mama Kanisa. Ni viongozi waliojitahidi kukesha, wakijitoa kimasomaso kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; ni watu ambao wamekuwa na mchango mkubwa wa mabadiliko ndani ya Kanisa mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, hawa ni viongozi ambao daima walishiriki Karamu ya Bwana na kwa sasa wanashiriki Karamu ya Yerusalemu ya Mbinguni. Sala ya Kanisa inalenga kuwaombea viongozi wote hawa ili kweli waweze kushiriki katika uzima wa milele, kielelezo cha ushindi wa Kristo dhidi ya nguvu ya kifo, kama alivyojionesha mwenyewe Siku ile ya Kwanza ya Juma, alipofufuka kutoka katika wafu.

Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanakufa na Kristo na wana matumaini kwamba, wataweza kuishi pamoja naye, kama alivyowaahidia; hili ni tumaini linalobubujika kutoka katika upendo wa Kristo; ni tumaini ambalo kamwe haliwezi kudanganya. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma kwa njia ya kifo cha Mwanaye mpendwa aliweza kuwapatanisha naye wakati walipokuwa wangali dhambini. Wanahesabiwa haki kutokana na imani yao kwa Yesu Kristo, Mtu mwenyehaki aliyetangazwa katika Maandiko Mataktifu na kwa njia ya Fumbo la Pasaka, waamini wanaweza kumwona Mwenyezi Mungu na hivyo kuuutafakari uso wake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, viongozi hawa wa Kanisa walipendwa kwa namna ya pekee na Bikira Maria, aliyewaonjesha upendo wa Kimama. Baba Mtakatifu anatumia fursa hii kumkabidhi roho za viongozi hao marehemu, ili aweze kuwaelekeza kwenye Ufalme wa Mungu, ambao waliufanyia kazi walipokuwa hapa duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.