Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika nia zake za jumla kwa Mwezi Novemba,
anayaelekeza mawazo yake kwa mihimili na wahudumu wakuu wa Injili ambao ni Maaskofu
na Mapadre kuwa na ujasiri kiasi cha kutolea ushuhuda makini na aminifu kwa Kristo
aliyeteswa, akafa na kufufuka. Kutujuvya zaidi ni Sr. Gisela Upendo Msuya.
Katika nia
zake za Kimissionari anawaalika waamini kuliombea Kanisa linalosafiri hapa duniani
liweze kung’ara miongoni mwa Mataifa, ili hatimaye, Mataifa yaweze kutembea katika
mwanga wake.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika barua yake kwa
Majandokasisi wakati wa kufunga Mwaka wa Mapadre, anasema kwamba, licha ya magumu,
changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zilizojitokeza katika maisha na utume wa
Kanisa, lakini bado kuna haja ya kuwa na Makleri wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya: Kutangaza Injili ya Kristo na Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba, hata katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya
sayansi na teknlojia, bado watu wataendelea kuwa na kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha
yao. Pale ambapo watu wanadhani kwamba, hawamhitaji Mungu, hapo kuna utupu na ubatili
na matokeo yake ni kinzani na vurugu za maisha ambazo zinaathari kubwa kwa maisha,
ustawi na maendeleo ya vijana. Baba Mtakatifu anasema Mungu ni hai na amemuumba na
anamfahamu kila mtu. Hata leo hii bado anaendelea kuita Mapadre watakaojitoa kimasomaso
kutangaza Injili ya Kristo hadi ukamilifu wa dahali.
Katika miaka ya hivi karibuni,
Kanisa limeshuhudia baadhi ya viongozi wake wakikumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa
kijinsia dhidi ya watoto wadogo; ni vitendo vya aibu na vilivyolipaka matope Kanisa,
kiasi cha baadhi ya watu kuhoji umuhimu wa useja na usafi wa moyo katika maisha ya
Kanisa. Licha ya vitendo vyote hivi anasema Baba Mtakatifu, bado wito na utume wa
Kipadre unahitajika. Hawa ni viongozi wenye imani hai inayoonesha ukomavu wao wa kiutu
hasa katika useja na usafi wa moyo. Ni changamoto ya kuwa makini kutambua na kuishi
wito wa maisha ya kipadre.
Makleri ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa wanaopaswa
kutolea ushuhuda wa Imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika
wafu. Sakramenti ya Daraja Takatifu ni kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo
kati ya wafuasi wake. Ni Kristo mwingine, changamoto ya kuhakikisha kwamba, matendo
na maisha yao yanamfanana Kristo, kwani kinyume chake ni ubatili mtupu!
Kutokana
na changamoto zote hizi, ndiyo maana Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika
waamini kuungana pamoja naye kusali kwa ajili ya kuwaombea Makleri, ili kweli waweze
kuwa ni wahudumu amini, wenye ujasiri wa kutolea ushuhuda wa kweli kuhusiana na maisha
na wito wao wa Kipadre, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika nia zake za Kimissionari kwa Mwezi Novemba,
2012, anawaalika waamini kuliombea Kanisa linalosafiri hapa duniani ili liweze kuwa
ni mwanga wa mataifa ili yaweze kutembea katika mwanga huu na hatimaye, kufikia utimilifu
wa maisha, kwa kuonesha umoja na mshikamano kama Familia ya Mungu. Kanisa katika hija
yake hapa duniani, linapania kuwaonesha watu njia inayokwenda kwa Kristo, Mkombozi
wa Ulimwengu. Kanisa linapania kuwa ni mhudumu wa kweli kwa binadamu, lakini zaidi
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Kila mtu anaalikwa
kuupokea mwaliko wa ukombozi na kwamba, kinzani na magumu yote yataponywa na hatimaye
kupata ukamilifu wake kwa kujipatanaisha na Kristo aliyemwaga damu yake Msalabani,
ili kumkirimia mwanadamu maisha yenye uzima wa milele. Ndiyo maana hata leo hii, Kristo
anaendelea kuita na kuwatuma watu kutangaza Ufalme wa Mungu, ili Mataifa yaweze kuwa
kweli ni Watu wa Mungu. Kwa Kanisa kutangaza Habari Njema ya Wokovu ni dhamana nyeti
na endelevu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa.
Kanisa
linalosafiri hapa duniani ni mbegu ya matumaini na mwendelezo wa huduma ya Kristo
kwa Walimwengu, ili waweze kufikia uzima wa milele; wakiendelea kusimama kidete kulinda
na kutetea haki, amani, uhuru, utu na heshima ya kila binadamu. Mama Kanisa anapania
kutangaza Injili ya Upendo hadi miisho ya dunia, ili mwanga wa Injili uweze kuleta
mabadiliko yanayokusudiwa kwa njia ya huduma na utume.
Mama Kanisa anaendelea
kuwaalika watu wote waweze kushiriki katika hija ya Wokovu iliyoanzishwa na Mwenyezi
Mungu kwa njia ya Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili. Ndiyo maana Kanisa bado linaendelea
kujikita katika Uinjilishaji wa Awali, miongoni mwa watu ambao bado hawajasikia Habari
Njema ya Wokovu, hadi pale kila kitu kitakapopata utimilifu wake ndani na kwa njia
ya Kristo Yesu.
Hii ni changamoto kwa Waamini kuendelea kutolea ushuhuda wa
Imani yao hata ikibidi kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Waamini
kwa namna ya pekee, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chumvi na mwanga
wa mataifa kwa kutambua kwamba, Uinjilishaji bado ni kati ya vipaumbele vya Mama Kanisa.