Mradi wa maboresho ya miji Tanzania wazinduliwa rasmi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi,
Novemba Mosi, 2012, amezindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya
Tanzania unaojulikana kama Mradi wa Uboreshaji Miji ya Tanzania (Tanzania Strategic
Cities project – TSCP) utakaogharimu mabilioni ya fedha.
Aidha, Rais Kikwete
amezidua rasmi Jiji la Arusha katika sherehe ya kufana iliyofanyika kwenye Mnara wa
Azimio la Arusha katikati ya jiji hilo. Mradi wa TSCP unalenga kuboresha huduma za
msingi katika miji saba na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kujenga
upya, kukarabati na kupanua miundombinu pamoja na kuijengea uwezo wa kukusanya na
kusimamia mapato ya miji husika.
Mradi ni moja ya miradi mitatu inayogharimiwa
na Benki ya Dunia kwa nia ya kuboresha miji ya Tanzania. Mbali na TSCP, miradi mingine
ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development
Project - DMDP) na Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP). Mpaka sasa
Benki hiyo imekwisha kutoa Sh. bilioni 8.76 kati ya Sh. bilioni 34.7 za TSCP.
Chini
ya TSCP ambao unagharimu kiasi cha Sh. bilioni 191.3 miji itakayonufaika ni Tanga,
Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya, Mtwara na CDA ambayo ndiyo itakayopata pesa
kubwa zaidi kuliko mjini mingine. Aidha, chini ya TSCP, miji hiyo itajengewa miundombinu
ya barabara zenye jumla ya kilomita 141.2, ujenzi wa madampo matano, ununuzi wa vifaa
vya kusimamia taka ngumu, vituo vya mabasi sita, vituo viwili vya kuegesha malori
na kilomita 15.9 za mitaro ya maji ya mvua.
Katika mji wa Arusha, kiasi cha
barabara za lami zenye urefu wa kilomita 7.23 zitajengwa, mtaro mkubwa wa maji ya
mvua wa mita 800 utajengwa, zitafungwa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara
tatu ambazo ni Sokoine na Viwandani, Sokoine na Esso na Kanali Middleton na Makongoro.
Katika awamu ya pili, kiasi cha barabara zenye urefu wa kilomita 7.8 zitajengwa katika
Jiji la Arusha.
Miji itakayonufaika na ULGSP ambako Benki ya Dunia inatoa mkopo
wa dola za Marekani milioni 255 na unatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha ni
Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba,
Lindi, Njombe, babati, Kibaha, Mpanda, Geita, Korogwe na Bariadi.
DMDP kwa
ajili ya Jiji la Dar Es Salaam, itahusika wilaya zote tatu za Kinondoni, Ilala na
Temeke na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 75. Baada ya kuzindua mradi
huo wa TSCP, Rais Kikwete amezindua Jiji la Arusha ambalo linapanda hadhi kutoka Manispaa.
Katika uzinduzi huo, Rais amezindua nembo ya Jiji pamoja na kukabidhi cheti cha kulipandisha
hadhi Jiji hilo.
Rais Kikwete amezindua miradi hiyo ikiwa ni shughuli zake
katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo
katika Mkoa wa Arusha. Rais amewasili Arusha mchana wa jana kutoka Dodoma.