TAFAKARI YA NENO LA MUNGU KATIKA SIKU YA KUWAKUMBUKA MAREHEMU WOTE
Ninakualika katika tafakari yetu tukiwakumbuka Marehemu wote. Kila mwaka tarehe 2
Novemba na zaidi sana mwezi Novemba ni siku na wakati ambao Mama Kanisa anatualika
kwa ajili ya kuwaombea marehemu walioko toharani.
Kwa kawaida
siku zote Mama Kanisa anasali kwa ajili ya marehemu mmojammoja au kikundi lakini leo
anasali kwa ajili ya Kanisa zima la wateswa lililoko toharani. Huo ndio utajiri wa
kanisa linapogawa mastahili ya msalaba wa Kristo kwa wahitaji walioko safarini kuelekea
mbinguni.
Mwanafalsafa John Mbiti alisema “Niko kwa sababu tuko na kwa
vile tuko, kwa hiyo niko ” Sentesi hii yanitafakarisha na kunisaidia kuhisi uwapo
wa mwingine pembeni mwangu aliye mhitaji na hivi yaonesha hitaji la jumuiya. Katika
siku ya leo Kanisa lahisi uwapo wa wahitaji ndio marehemu wote, ndio waliolala toharani
wakitakaswa ili waingie mbinguni. Kanisa lahisi na kutekeleza ule muunganiko uliopo
kati ya marehemu (Kanisa la wateswa), watakatifu wa mbinguni (Kanisa la washindi)
na kanisa la wapiganaji ndio sisi na hivi kwa pamoja ni kanisa moja familia ya Mungu.
Fundisho
tulilolisikia juu ya muunganiko wa kanisa shindi, Kanisa la wateswa na Kanisa la
mahujaji linawekwa mbele yetu na Papa Paulo VI akisema “sisi twasadiki ushirika wa
waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao
wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya kanisa moja tu.
Nasi twasadiki kwamba katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu
wake yasikiliza daima sala zetu” (KKK 962) Ndiyo kusema kuwaombea marehemu ni sehemu
ya imani yetu, ni upendo kwa jirani tukiitikia injili ya Bwana ya kumsaidia aliye
katika taabu, aliyemhitaji.
Kuwaombea marehemu ni kielelezo kimojawapo cha
imani yetu katika ufufuko, kwa maana kama hatusadiki yakuwa Kristu alikufa na kufufuka
imani yetu ni bure. Ni kutokana na msingi huo twaamini kwamba wale waliolala usingizi
katika Yesu Kristu mfufuka, parapanda ya Mungu ikilia watafufuliwa kwanza nasi tuliosalia
tutanyakuliwa kwa kuwafuata wao.
Kuwaombea marehemu ni jambo la thamani na
la imani ambalo si la leo bali limekuwepo katika safari ya wokovu. Tunasoma daima
katika kitabu cha pili cha Wamakabayo kuwa Yuda kiongozi wa Wayahudi alichanga fedha
kwa kila mtu jumla drakma mbili elfu, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi.
Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Alifanya
hili kwa sababu ya imani na kama asingekuwa na imani kuwa wafu watafufuliwa ingekuwa
upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. (Rej. 2Wak. 12: 43-45).
Basi ndugu
yangu mpendwa ninakualika katika msingi uleule wa imani katika ufufuko, kusali daima
sala hii “Raha ya milele uwape Ee Bwana na mwanga wa milele uwaangazie wapumzike
kwa amani, amina”. Ni Sala ya kujenga urafiki na marehemu walioko toharani
na hatimaye watakatifu wa mbinguni. Ni sala ambayo yatukumbusha wapendwa wetu ambao
wengine tuliwafahamu kwa karibu na hivi yatudai wajibu wa kuomba huruma ya Mungu kwa
ajili yao pasipo kukoma.
Mama kanisa ametuwekea Misa tatu kwa ajili ya marehemu
wote ili kwa njia hiyo marehemu wapate msaada wa masitahili ya Kristu kwa njia sadaka
yake ya msalabani. Anataka asiwepo hata mmoja atakayekosa huruma na msaada wa Mungu.
Katika Misa hizi tatu injili zagusa Heri Nane njia ya utakatifu na habari
ya ufufuko wa wafu lililotumaini letu na imani yetu tunaposafiri kuelekea ukamilifu
yaani uzima wa milele ambao huja baada ya kifo. Tunasali na kutumaini kuwa, kwa kifo
maisha hayaondolewi ila hugeuzwa na kuwa maisha mapya, maisha makamilifu.
Basi
mpendwa mwanatafakari, leo ni wakati wa kusali na kuwatembelea waliolala kule makaburini
ili muunganiko katika sala ukamilishwe katika upendo unaoonekana katika maisha ya
watu. Yafaa pia kufunga kidogo kwa ajili ya wapendwa wetu ili kuisimika sala yetu
katika majitoleo ya Kristo mteswa na hatimaye uibuke na ushindi wa Kristu mfufuka.
Kumbukeni pia kujiombea wewe mwenyewe kwa maana kwakukumbusha kujitayarisha kwa ajili
ya safari ya kugeuzwa na kuingia maisha mapya, maisha ya mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S., Roma.