2012-11-01 10:44:53

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kiwe ni kipimo cha Uinjilishaji Mpya ili kukoleza Imani ya Kikristo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati alipokuwa anafunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya alikazia kwamba, Watakatifu ni Wainjilishaji Wakuu, kwani wao wamebahatika kuzungumza lugha inayoeleweka na watu wa nyakati mbali mbali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yaliyojionesha kwa namna ya pekee, katika matendo ya huruma.

Kutokana na changamoto hii anasema Askofu Mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya kwamba, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya wamekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa waamini kujikita katika maisha ya Kisakramenti, Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu ambao bado hawajasilia Neno la Mungu likitangazwa katika maisha yao pamoja na kuleta mwamko mpya kwa Wakristo wale ambao Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake inaonekana kupooza kutokana na kumezwa mno na malimwengu.

Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanataka ifanyiwe kazi na Makanisa mahalia katika mchakato mzima unaopania kutangaza na kumwilisha Imani ya Kikristo kama ambavyo anaendelea kukazia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Idara ya Katekesi kwa sasa itakuwa chini ya uongozi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya, changamoto kubwa iliyoko mbele yao anasema Askofu mkuu Fisichella ni kuhakikisha kwamba, Wadau wa Katekesi wanaandaliwa barabara, ili waweze kufahamu kwa kina na mapana kile wanachopaswa kufundisha, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya Uinjilishaji Mpya na Katekesi. Ni wakati muafaka kwa Wakristo kutambua Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili kuwasaidia wale ambao wanatembea katika Jangwa na maisha ya kiroho, waweze kupata kitulizo na hatimaye, kuzima kiu yao kutoka kwa Kristo, Mwanga wa Mataifa.

Jangwa na utupu wa maisha unajionesha kwa namna ya pekee katika: matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi, ukahaba, hali ya kukata tamaa inayopelekea vijana wengi kujikuta wanatumiwa na baadhi ya wanasiasa waliofilisika kimaadili na kiutu kuchochea vurugu na ghasia kwa ajili ya mafao ya wanasiasa hao. Ni Jangwa linalogusa tatizo la ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana, kiasi kwamba, hawana tena matumaini thabiti kwa kesho iliyo bora zaidi.

Waamini wanapaswa kutoa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa maisha na wito wa Familia kwa ajili ya mafao ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, kwani hapa ni mahali pa kwanza kabisa pa kurithisha Imani, Kweli za Kiinjili, tunu bora za kijamii na kimaadili. Ni wakati kwa Mama Kanisa kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji Mpya, wajibu ambao unafumbatwa katika maisha ya kila mwamini kutokana na dhamana na wajibu aliojitwalia wakati wa Ubatizo, kuzima kiu ya watu wanaomtafuta Mungu.

Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni kati ya mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuona kwamba, watu wanahitaji Kuinjilishwa Upya kutokana na kumezwa sana na malimwengu, kutawaliwa na mawazo mepesi mepesi na ukanimungu, mambo ambayo hayana tija katika ukuaji wa Imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Mababa wa Sinodi wamebainisha kwamba, athari hizi zinatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine, kumbe ni wajibu na dhamana endelevu kwa Makanisa mahalia kusoma alama za nyakati na kutafuta jibu muafaka kutokana na changamoto, magumu na fursa wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao ya Kiimani, Kichungaji na Kitamaduni.

Uinjilishaji Mpya anasema Askofu mkuu Rino Fisichella kwamba, ni changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuanzia kwa viongozi wa Kanisa na watu wenye dhamana mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa, kuhakikisha kwamba, wanafanya uchunguzi wa dhamiri ili kubainisha matatizo, changamoto na fursa walizonazo katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya. Ni mwaliko wa kutafuta mbinu na njia mpya ili kutangaza Imani ya Kikristo kwa nguvu na ari kubwa zaidi.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kiwe ni kipimo cha Uinjilishaji Mpya, ili kutoa mwelekeo mpya wa Imani inayotangazwa, adhimishwa na kumwilishwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.