Wakenya: salini ili kuombea uchaguzi mkuu, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa!
Askofu Salesius Mugambi wa Jimbo Katoliki Meru, Kenya, Jumapili iliyopita, tarehe
28 Oktoba 2012, wakati wa maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, aliwaalika waamini na
wananchi wa Kenya katika ujumla wao, kuombea uchaguzi nchini humo, unaotarajiwa kufanyika
hapo tarehe 4 Marchi 2013, ili uweze kuwa: huru, wa haki, amani na utulivu sanjari
na kuombea maboresho ya ulinzi na usalama nchini Kenya.
Jumapili iliyopita
ilikuwa ni Siku ya kusali kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya Vikosi vya Ulinzi
na Usalama na Familia zao nchini Kenya na imeongozwa na kauli mbiu "Ili wote wawe
wamoja". Askofu Mugambi ambaye amewataka Wanajeshi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama
kutekeleza wajibu wao kwa umakini na uchaji mkubwa, daima wakimtegemea Mwenyezi Mungu
katika maisha yao ya kila siku.
Kwa njia hii, Kenya inaweza kugeuka na kuwa
kweli ni nchi ya Wachamungu, changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kuanzia kwenye Familia
na katika maeneo mbali mbali ya kazi, lengo ni kuyatakatifuza malimwengu.
Itakumbukwa
kwamba, kabla ya mabadiliko yaliyofanyika kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya,
mshauri wa kiroho kwa Wanajeshi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini Kenya, alikuwa
ni Askofu Philip Anyolo, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa ni Makamu wa Rais
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya. Yeye alifanya utume huu kwa takribani miaka kumi
na minne na kwa hakika anastahili kupewa pongezi za dhati.
Kwa upande wake,
Askofu Anyolo amemtakia ufanisi, tija na mafanikio mema katika utumishi wake huu mpya
kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama na anawaalika wanajeshi kuunga mkono juhudi
za Kanisa katika kulinda, kutetea na kuimarisha: haki, amani, upendo na mshikamano
wa kitaifa miongoni mwa wananchi wa Kenya.
Akizungumza katika maadhimisho haya,
Rais Mwai Kibaki, Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini Kenya, amelishukuru
Kanisa kwa huduma ya maisha ya kiroho wanayoitoa katika vikosi vya ulinzi na usalama.
Amekazia zaidi nidhamu na umakini kwa wanajeshi; daima wakijitahidi kujenga na kuimarisha
mshikamano na umoja wa kitaifa ambao kwa miaka ya hivi karibuni ulitikiswa vibaya
sana, lakini zaidi, wakati huu, Kenya inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Ni
matumaini ya Rais Kibaki kwamba, Kanisa nchini Kenya, litaendelea kuchangia kwa hali
na mali katika kukuza na kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwa wanajeshi
wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa makini na watu wanaotaka kuwagawa Wakenya kwa masilahi
yao binafsi.