2012-10-31 08:36:06

Michoro ya Kikanisa cha Sistina inaadhimisha Jubilee ya Karne Tano, tangu ichorwe na Msanii maarufu Michelangelo


Ilikuwa ni tarehe 31 Oktoba 1512, takribani karne tano zilizopita, wakati ambapo Baba Mtakatifu Giulio II alipokuwa anafungua rasmi Kikanisa cha Sistina, ambacho kimekuwa ni maarufu sana na kivutio kikuu cha watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaobahatika kufika hapa mjini Vatican.

Hiki ni Kikanisa kilichopambwa kwa michoro ya Msanii maarufu sana Michelangelo, mtu ambaye alileta mabadiliko makubwa katika historia ya sanaa za Italia na Ulaya katika ujumla wake. Hii ni kazi ya miaka minne, iliyoanza kufanyika kunako mwaka 1508 hadi mwaka 1512.

Takwimu kutoka Vatican zinaonesha kwamba, kila mwaka walau kuna jumla ya watu millioni tano wanaotembelea Makumbusho ya Vatican, lakini zaidi kwenye Kikanisa cha Sistina. Kila siku, walau kuna watu zaidi ya elfu ishirini wanaotembelea Makumbusho ya Vatican.

Idadi ingeweza kuongezeka maradufu, lakini kutokana na ushauri wa kitaalam, kiasi hiki cha watu ndicho kinachoruhusiwa kuingia na kujionea utajiri wa sanaa unaogusa vionjo vya mwanadamu. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika hifadhi ya Kumbukumbu za Kale, pengine kwa siku za usoni, idadi ya watalii ikaongezeka maradufu.

Kutokana na tukio hili la kihistoria, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano jioni, tarehe 31 Oktoba 2012 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya jioni kwa ajili ya Maadhimisho ya Jubilee ya Karne Tano ya Michoro ya Kikanisa cha Sistina.







All the contents on this site are copyrighted ©.