Vatican na Croatia kuendelea kushirikiana kwa ajili ya mafao ya pande hizi mbili
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu tarehe 29 Oktoba 2012 amekutana
na kufanya mazungumzo na Bi Zoran Milanovic, Waziri mkuu wa Croatia pamoja na ujumbe
wake. Viongozi hawa wawili wametumia fursa hii kubadilishana mawazo na changamoto
ambazo Croatia inakabiliana nazo kwa wakati huu kutokana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Wamegusia masuala yenye mafao kwa pande hizi mbili.
Wamezungumzia
pia kuhusu Kongamano lililoandaliwa na Croatia kwa kushirikiana na Vatican kama sehemu
ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka ishirini ya uhusiano kati ya Vatican na Croatia,
lililofanyika Jumatatu tarehe 29 Oktoba, 2012. Viongozi hawa pia wamekubaliana kimsingi
kulipatia ufumbuzi tatizo la Dajla katika hali ya mapokeo ya kirafiki kati ya Vatican
na Croatia.
Baba Mtakatifu amemhakikishia mgeni wake kwamba, Vatican itaendelea
kuunga mkono jitihada zinazolenga kuiwezesha Croatia kujiunga na Umoja wa Ulaya, bila
kusahau hali halisi ya wananchi wa Croatia walioko Bosnia na Erzegovina.
Waziri
mkuu Zoran Milanovic na ujumbe wake, walipata pia fursa ya kukutana na viongozi waandamizi
kutoka Vatican chini ya uongozi wa Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.