2012-10-30 09:59:02

Mwaka wa Imani iwe ni fursa ya kujichotea utajiri unaobubujika katika Sala, Sakramenti, Neno la Mungu na Huduma ya Upendo


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wanazialika kwa namna ya pekee Familia za Kikristo kuweza kujichotea utajiri unaopatikana katika maisha ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Katekesi na Matendo ya huruma.

Lengo kuzijengea Familia za Kikristo uwezo wa kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani, zikitambua kwamba, zina mchango mkubwa katika dhamana ya Mama Kanisa katika Uinjilishaji Mpya, dhana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Maaskofu wanazichangamotisha Familia kuhakikisha kwamba, zinajenga na kuimarisha moyo wa Sala na Tafakari ya Kina, ili kujenga na kuimarisha Familia ili iweze kuwa kweli ni Kanisa Dogo la Nyumbani, changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Wazazi na walezi wajenge utamaduni wa kusali walau zile sala za kawaida na watoto wao katika matukio mbali mbali ya maisha, wakitambua na kuthamini kwanza kabisa Sala ya Kanisa ambayo ni kwa ajili ya waamini wote na wala si kikundi cha Mapadre na Watawa tu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni fursa makini kabisa kwa Familia kupata mwamko na ari mpya katika maisha na utume wao kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla. Familia zioneshe kwa njia ya ushuhuda wa maisha na vipaumbele vyao umuhimu wa kuwa kweli ni Mfuasi wa Kristo.

Familia zijenge utamaduni wa kukutana na Yesu Kristo katika maadhimisho ya Sakramenti na Ibada mbali mbali za Kanisa, lakini nafasi ya pekee iwe ni katika Maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, Sakramenti ya Upatanisho, mahali ambapo Familia inajichotea huruma na upendo wa Mungu, ikihamasishwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kama mwaliko wa kwanza kabisa wa wafuasi wa Kristo bila kusahau Neno la Mungu ambalo ni ufunuo na muhtasari wa kazi nzima ya Ukombozi.

Wazazi na walezi wawe ni Makatekista wa kwanza wa imani, maadili na utu wema. Ili kutekeleza wajibu huu nyeti, wanapaswa kwa hakika kujitaabisha zaidi na zaidi kupenda kujisomea na kutafakari kwa kina Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Sala za Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanatarajiwa kufungwa hapo tarehe 24 Novemba 2013, wakati Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Dunia. Mwaka wa Imani ni matokeo ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Kumbu kumbu ya Miaka ishirini, tangu Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo.

Zote hizi ni fursa kwa Waamini kutubu, kuongoka, kuchuchumilia utakatifu wa maisha na kutolea ushuhuda makini na wenye mvuto imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.