2012-10-29 09:36:39

Uvumilivu, utulivu, busara, imani na matumaini vinahitajika ili kufikia upatanisho wa kweli kati ya Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio wa Kumi na Kanisa


Tume ya Kipapa ya Kanisa la Mungu, inakubaliana kimsingi na ombi lililotolewa hivi karibuni na Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio wa kumi, ikionesha kwamba, inahitaji kupata muda mrefu zaidi, ili iweze kufanya tafakari ya kina, kupembua na kusali, kuhusu msimamo uliokuwa umetolewa na Vatican kuhusu mgogoro na hali ya kutoelewana iliyojitokeza kati ya Jumuiya hii na Vatican.

Hali iliyofikiwa kwa wakati huu ni matunda ya majadiliano ya kina kati ya Vatican na Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio wa kumi, ambayo yamedumu kwa takribani miaka mitatu, yakijikita zaidi katika: Mafundisho tanzu ya Kanisa na Taalimungu. Tume inayojumuisha wawakilishi kutoka pande hizi mbili, imekwisha kukutana mara nane kujadiliana kwa kina kuhusu msimamo na tafsiri yao kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Baada ya muafaka kupatikana, hatua iliyokuwa inafuata ni utekelezaji wa moja kwa moja unaopania kujikita katika upatanisho kati ya Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio wa kumi pamoja na Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameonesha upendo wa kibaba katika mchakato wa upatanisho unaolenga kuponya madonda ya utengano kunako mwaka 2009. Tarehe 13 Juni 2012 Jumuiya hii ilionesha kukubaliana kimsingi na Kanisa kuhusu Mafundisho Tanzu na kwamba, walikuwa sasa wanaendelea kutafakari jinsi ya kujipatanisha na Kanisa mintarafu Sheria za Kanisa.

Tume ya Kipapa ya Kanisa la Mungu inaendelea kuvuta subira ili Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio wa kumi iweze kutoa tamko lake rasmi, baada ya kuwa imejitenga na Kanisa kwa miaka thelathini. Ni subira ya kichungaji inayooneshwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anayepeania kwa namna ya pekee kabisa, kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa, ili wote waweze kujisikia kuwa chini ya mchungaji wao mkuu Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ili kufikia lengo hili bado kuna haja kuonesha uvumilivu, subira, utulivu wa ndani, imani na matumaini katika mchakato huu ambao umepitia pia kipindi kigumu chenye majaribu na hali ya kukatisha tamaa.







All the contents on this site are copyrighted ©.