2012-10-29 08:07:27

Mshikamano wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa waathirika wa Majanga asilia sehemu mbali mbali za dunia!


Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumapili tarehe 28 Oktoba 2012, aliyaelekeza mawazo yake nchini Cuba, Haiti, Jamaica na Bahamas, nchi ambazo kwa siku za hivi karibuni zimekumbwa na tufani kubwa iliyosababisha madhara makubwa kwa maisha na mali za watu. Tufani hii anasema Baba Mtakatifu imesababisha watu wengi kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anachukua fursa hii, kuwahakikishia wote waliokumbwa na maafa haya asilia kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala na kwamba, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya watu waliokumbwa na maafa haya sanjari na kuonesha mshikamano wa upendo kwa njia ya msaada wa hali na mali.

Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa Italia wanaoishi kwenye maeneo ya Basilicata na Calabria yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi pamoja na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyeesha sehemu mbali mbali za Italia kwamba, yuko pamoja nao katika shida na mahangaiko yao kwa wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.