Mababa wa Sinodi wameonesha unyenyekevu wa hali ya juu, daima wamejitahidi kusoma
alama za nyakati, sasa ni kipindi cha kumwilisha changamoto hizi katika maisha na
utume wa Kanisa!
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya katika ujumbe wao kwa Watu wa
Mungu sehemu mbali mbali za dunia, wanawahimiza waamini kwa namna ya pekee, kuhakikisha
kwamba, wanauhisha imani yao ili isimezwe na malimwengu. Wajitahidi kutafuta fursa
za kukutana na Mwenyezi Mungu anayejifunua kwa namna ya pekee, kama kielelezo cha
upendo unaojidhihirisha ndani ya Kanisa kama Jumuiya inayosimikwa katika misingi ya
Umoja na Mshikamano.
Kutokana na
dhamana hii, Waamini wanaalikwa kutolea ushuhuda umoja uliopo kati yao. Mababa wa
Sinodi wanabainisha kwamba, ili Wakristo waweze Kuinjilisha, kwanza kabisa hawana
budi Kujiinjilisha wao wenyewe, ili ujumbe wao uweze kuwa na mvuto pamoja na mguso
kwa wale watakaokutana nao katika hija ya maisha yao. Jambo la msingi ni kuhakikisha
kwamba, wanajikita katika toba na wongofu wa ndani unaowawezesha kuyaona, kukiri na
hatimaye, kujiwekea mikakati ya maboresho katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya.
Askofu
Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania alikuwa Mwakilishi wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania waliokuwa wanahudhuria kwenye Maadhimisho ya Sinodi
ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumkirimia fursa
hii ya kuweza kusali, kutafakari, kusikiliza na kushirikishana mang’amuzi, changamoto,
fursa na matumaini ya Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo.
Askofu Libena anasema,
jambo ambalo limemgusa kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji
Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo ni jinsi ambavyo Mababa wa Sinodi walivyoonesha
unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, kwa kusoma alama za nyakati, wakitambua kwamba,
huu ndio muda muafaka wa kuamsha ari na mwamko katika azma ya Uinjilishaji Mpya; kwa
kukazia toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha; kwa kujikosoa na kukosoa, ili
kuibua mbinu mkakati unaopania maboresho ya Uinjilishaji Mpya, kama sehemu ya utekelezaji
wa Agizo la Kristo la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Dhamana
ya Uinjilishaji Mpya ni changamoto inayotakiwa kwanza kabisa kutekelezwa na Wainjilishaji
mihimili ili waweze kuinjilisha kwa umakini mkubwa na kwamba, Uinjilishaji ni wajibu
fungamanishi kwa Wafuasi wote wa Kristo.
Mababa wa Sinodi wamekiri kwa unyenyekevu
kwamba, katika maeneo ambayo Kanisa halijafanya vyema sana ni katika maadhimisho ya
Liturujia ya Kanisa. Wakristo wanapaswa kujipanga vyema na kwa umakini mkubwa ili
maadhimisho haya yaweze kuleta mvuto na mguso kwa makundi ya vijana na wanaume ambao
mara nyingi wamekuwa wakisua sua katika kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.
Mahubiri yaandaliwe kwa usafaha na maadhimisho ya Liturujia mbali mbali za Kanisa
yamguse mwamini katika undani wa maisha yake: kiroho na kimwili.
Mababa wa
Sinodi anasema Askofu Libena kwamba, wamekazia na kuwahimiza Waamini kujichotea utajiri
unaobubujika kutoka katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya
Kanisa na Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mwaka wa Imani uwe ni fursa
ya kuimarisha Imani kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda makini.